WATU 25 WAUWAWA UKRAINE
Licha ya kuuawa kwa watu zaidi ya 20
na wengine zaidi ya 200 kujeruhiwa usiku wa kuamkia leo mjini Kiev,
waandamanaji wameapa kurudi kwenye Uwanja wa Uhuru kuendelea kushinikiza
kujiuzulu.
Rais Viktor Yanukovych huku rais huyo
anawalalamikia viongozi wa upinzani kutokana na vurugu hizo kati ya
polisi na waandamaji na kutishia kuchukua hatua kali zaidi.
Moshi, vilio na hasira ndiyo picha ya
mji mkuu wa Ukraine, Kiev, asubuhi ya leo, baada ya vurugu zilizotekea
jana, ambazo zinatajwa kuwa mbaya zaidi kutokea katika maandamano ya
kupinga serikali ya Kiev, ambayo yamedumu kwa karibu miezi mitatu na
kukwamisha shughuli mbalimbali mjini humo. Maelfu ya polisi wa kutuliza
ghasia waliokuwa na maguruneti na maji ya kuwasha waliwashambulia
waandamanaji katika kambi yao mjini Kiev.
Kiongozi wa upinzani Vitali Klitschko
amewataka waandamanaji kiasi cha 20,000 kwenda kuulinda uwanja wa Uhuru
ambao umekuwa kitovu cha maandamano hayo, na ambao kwa sasa robo tatu
inashikiliwa na polisi:
Kiongozi huyo ambae ni bingwa wa
zamani wa ndondi za uzito wa juu aliwaambia waandamanaji kuwa
hawataondoka katika eneo la kambi ya maandamano kwa kusema hicho ni
kisiwa cha uhuru na watakilinda kwa kadiri wawezavyo.
Waandamanaji watoa kauli kali
Mapema leo wengi wa raia wameonekana
kusikiliza wito wa kiongozi huyo. Mwanandamaji mmoja, Anthony
Rybkovivich, mwenye umri wa miaka 32 amesikika akisema "Sitokwenda kukaa
tu na kusubiri niuwawe, nakwenda kupambana."
Kiasi ya watu 10,000 wameendelea
kubakia katika uwanja huo wakati moto uliowashwa kwa kutumia matairi
ukiendelea kuwaka. Jengo kubwa ambalo waandamanaji wamekuwa wakilitumia
kama makao makuu limewaka moto na limetelekezwa wakati wa vurugu za
usiku pale ambapo polisi walipotumia kipaza sauti kutangaza wanawake na
watoto waondoke katika uwanja huo kwa kile walichosema kunafanyika
operesheni ya kukabiliana na magaidi.
Upinzani walaumiwa kwa vurugu
Rais Yanukovych anasema viongozi wa
upinzani wamevuuka mipaka kwa kutoa wito kwa watu kubeba silaha. Katika
taarifa yake, kiongozi huyo ameutaka upinzani kujitenga na makundi ya
wenye itikadi kali wanachochea vitendo vya umwagikaji damu na vurugu
dhidi ya vikosi vya usalama.
Aidha Yanukovych aliongeza kusema kuwa
endapo hawataondoka katika uwanja wa maandamano wataonekana kama wenye
kuunga mkono misimamo ya wenye itikadi kali. Na kwa hivyo ameonya kwamba
mazungumzo baina yao yanaweza kubadilika muelekeo wake.
Viongozi mbalimbali wa kimataifa
wamepaza sauti zao juu ya hali ya mambo nchini Ukraine. Makamu wa Rais
wa Marekani, Joe Biden, ameonesha kusikitishwa kwake wakati
alipozungumza na Yanukovych kwa njia ya simu. Huku sauti nyingine kutoka
huko zikitoa wito wa taifa hilo kuwekewa vikwazo wazo ambalo limepingwa
na Ujerumani.
Chanzo, dw.de.com
No comments:
Post a Comment