MBEKI NA JUHUDI ZA KUSAKA AMANI SUDAN
Rais Salva Kiir,waziri mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn ba mpatanishi Thabo Mbeki
Mpatanishi mkuu wa Umoja wa Afrika
kuhusu mgogoro wa Sudan,Thabo Mbeki anafanya ziara mjini Khartoum akiwa
na lengo la kusaidia kutia msukumo katika juhudi za kutafuta amani kati
ya serikali ya Sudan na SPLM-N.
Ziara hiyo ya Mbeki inafanyika kabla ya mazungumzo yanayotarajiwa kuanza tena mjini Ethiopia siku ya Ijumaa 28.02.2014.
Mpatanishi mkuu wa Umoja wa Afrika
katika mgogoro wa Sudan Thabo Mbeki anaianza ziara yake hiyo ya mjini
Khartoum ikiwa tayari serikali ya Sudan na waasi wa Kordofan Kusini
wameridhia kusitisha mapigano na kuruhusu msaada kuwafikia zaidi ya watu
milioni 1 kwa mujibu wa makubaliano yaliyopendekezwa kabla ya kuvunjika
mazungumzo ya kusaka amani wiki iliyopita.Itakumbukwa kwamba katika
mkutano huo wiki iliyopita,wajumbe wa Umoja wa Afrika waliwasilisha
pendekezo hilo kwa serikali ya Khartoum na waasi hao wa kundi la SPLM-N
kabla ya mazungumzo hayo ya mjini Adis Ababa kuakhirishwa kutokana na
pande hizo mbili kutupiana lawama.
Mpatanishi mkuu,wiki iliyopita alisema
wajumbe kutoka upande wa waasi na serikali watabidi kushauriana na
kundi la wapatanishi kuhusiana na mapendekezo hayo ya Umoja wa Afrika
ingawa pia hakutowa maelezo zaidi kuhusiana na suala hilo. Kimsingi sasa
mazungumzo hayo yanasubiriwa kuanza tena tarehe 28 mwezi huu wa
Februari. Katika kikao cha mwanzo mjini Adis mkuu wa ujumbe wa waasi
Yassir Armen alisema serikali ya Sudan inataka kumaliza vita hivi bila
ya kutowa suluhisho katika suala zima la hali ya kibinadamu na kisiasa.
Kwa upande wake serikali ya Khartoum
inalishutumu kundi hilo la waasi wa SPLM-N kwa kuongeza masuala ambayo
hayahusiani na migogoro ya Kordofan Kusini na jimbo la Blue Nile.
Mgogoro na uhasama wa kikabila katika majimbo hayo mawili pamoja na uasi
wa muda mrefu katika jimbo la Darfur yametokana na malalamiko ya
kiuchumi pamoja na kutengwa kisiasa kwa majimbo hayo na utawala wa
Khartoum unaohodhiwa na waarabu.
Ni kutokana na hali hii rais wa zamani
wa Afrika Kusini ambaye sasa ni mpatanishi mkuu wa Umoja wa Afrika
katika mzozo huu anataka kuzipa msukumo juhudi za kupatikana mwafaka wa
amani baina ya pande hizo mbili zinazozana huku pia ukitarajiwa
kufanyika mkutano wa tume ya pamoja ya Kimataifa iliyoundwa chini ya
makubaliano ya amani ya mwaka 2011 kati ya Khartoum na muungano wa
makundi ya waasi yaliyojitenga.Tume hiyo ilipewa jukumu la kufuatilia
maendeleo ya makubaliano hayo.
Chanzo, dw.de.com/swahili. R.M
No comments:
Post a Comment