RWANDA YAPONGEZA HUKUMU YA RWABUKOMBE HUKO UJERUMANI
Mahakama moja ya Ujerumani imemhukumu
meya wa zamani wa Rwanda, Onesphore Rwabukombe, kifungo cha miaka 14
gerezani kwa jukumu lake katika mauaji ya halaiki ya mwaka 1994 ya
Rwanda.
Rwabukombe mwenye umri wa miaka 56
alikutwa na hatia ya kuamuru mauwaji ya mamia ya watu katika kanisa moja
ambako watu walikusanyika kupata hifadhi huko Kiziguro. Amekuwa akiishi
kama mkimbizi wa kisiasa nchini Ujerumani tangu mwaka 2002.
Hii ni kesi ya kwanza kufanyika
Ujerumani iliyohusisha mauaji ya halaiki nchini Rwanda. Kesi hiyo
iliyodumu miaka mitatu huko Frankfurt ilisikiliza ushahidi kutoka zaidi
ya mashahidi 100 na wapelelezi wa jinai walipelekwa Rwanda kufanya
uchunguzi.
Serikali ya Rwanda imepongeza uamuzi wa mahakama ya Frankfurt, kumhukumu Rwabukombe mshukiwa wa mauaji ya Rwanda mwaka 1994.Rwanda inasema hata kama kesi hiyo imesikilizwa nje ya nchi lakini ni ishara kwamba sheria za kimataifa zinaheshimiwa popote pale unapokimbilia.
Kesi ilisikiliza namna kati ya watu 400 hadi 1,200 walivyouwawa hapo April 11 mwaka 1994 kwenye kanisa moja huko Kiziguro, mashariki mwa Rwanda ambako Rwabukombe wakati huo alikuwa meya.
Mwendesha mashtaka mkuu Christian Ritcher alisema Ujerumani sio mahala pa hifadhi ya watenda maovu kufuatana na sheria za kimataifa anasema huo ndio ujumbe ambao umetolewa jumanne kwa sauti kubwa kufuatia hukumu hii.
Rwabukombe alikana mashtaka yote. Mawakili wake wamesema walitaka kesi ifutiliwe mbali na wamesema watakata rufaa.
Kuna baadhi ya nchi zilizowafungulia mashtaka washukiwa wa Rwanda katika nchi walizokimbilia lakini Kigali inataka washukiwa walio nje ya nchi kurudishwa nyumbani na kupatiwa hukumu kwenye nchi yao na inasisitiza washukiwa hao kurudishwa nyumbani.
Mataifa mengi yangali yanasita kuchukua hatua hiyo . Watu watano huko Uingereza wanasubiri kesi ya kusafirishwa nyumbani inayotarajiwa kuanza wiki ijayo.
Chanzo, voaswahili.com/
No comments:
Post a Comment