TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Tuesday, April 21, 2015

Ethiopia yaanza siku 3 za maombolezi 

Islamic State wakienda kuwaua raia wa Ethiopia.
Ethiopia imeanza siku tatu za maombolezi ya kitaifa kwa heshima za raia wake waliouawa na wanamgambo wa kundi la Islamic State nchini Libya.
Bendera zitapepea nusu mlingoti wakati nalo bunge la nchi hiyo likikutana kujadili hatua ambazo litachukua kufuatia mauaji hayo ya raia wake zaidi ya ishirini.
Msemaji wa serikali Redwan Hussein, alisema kuwa waathiriwa hao wanaaminika kuwa wahamiaji waliojaribu kusafiri kwenda barani ulaya.
Mungano wa Afrika ambao una makao yake makuu nchini Ethiopia ulilaani mauaji hayo na kusema kuwa utafanya mikakati ya kuhakikisha kuwepo usalama nchini Libya.
Wanamgambo wa Islamic State walitoa kanda ya video ambayo inakisiwa kuonyesha mauaji hayo yanayoonyesha watu hao wakipigwa risasi na kukatwa vichwa.CHANZO:BBC(V.S)

Mwanafunzi darasa la nne ajinyonga chumbani 

MWANAFUNZI wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Pugu jijini Dar es Salaam, Festo Filbert (11) amekutwa chumbani kwake akiwa amejinyonga hadi kufa kwa kutumia mkanda wa kuvalia nguo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Mary Nzuki alisema tukio hilo lilitokea jana katika eneo la Majohe kwa Ngozoma.
Alisema sababu za kujinyonga mwanafunzi huyo bado hazijafahamika kwani hakuacha ujumbe wowote.
"Mtoto huyu alikutwa chumbani kwake anakolala akiwa peke yake, hakuna aliyejua sababu za kifo chake," alisema.
Alisema maiti ya mwanafunzi huyo, imehifadhiwa Hospitali ya Amana na polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.CHANZO:MTANZANIA (Muro)

Majimbo yapasua kichwa wana-Ukawa

Mwenyekiti wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba.
Mwenyekiti wa Ukawa, Profesa Ibrahim Libumba.
HATIMA ya kuachiana kwa majimbo ya uchaguzi kwa vyama vya siasa vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), inatarajiwa kujulikana wiki ijayo.
Itajulikana baada ya mkutano baina vyama washirika, uliolenga kutaka kufikiwa kwa mwafaka wa ugawanaji wa majimbo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Hayo yamethibitishwa na mmoja wa viongozi wa Ukawa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba.
Vyama vingine vinavyounda umoja huo ni Chadema inayoongozwa na Freeman Mbowe, NCCRMageuzi ya James Mbatia na NLD ya Dk Emmanuel Makaidi.
Alikuwa akizungumza na gazeti hili juzi mjini hapa juu ya mchakato wa makubaliano ya majimbo, ambayo baadhi yamezua mvutano ndani ya Ukawa. Kwa Lipumba, suala hilo limepangwa kumalizwa Aprili 28, mwaka huu jijini Dar es Salaam, ambapo viongozi vinavyounda umoja huo vitatu watakutana.
Aliwataja viongozi kutoka vyama hivyo, watakaohusika katika majadiliano ya kina ni pamoja na wenyeviti wa vyama, makamu wenyeviti, makatibu na wajumbe wa sekretarieti kutoka ndani ya vyama hivyo watakuja kufikia makubaliano ya mwisho.
Ukawa ulianzishwa Februari mwaka jana wakati wa Bunge Maalumu la Katiba baada ya kushikamana katika kulipinga bunge hilo la kihistoria na baadaye kususa, kabla ya kusaini makubaliano kwa ajili ya kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi zote kuanzia udiwani, ubunge na urais.
Hata hivyo, Lipumba alisema baada ya majadiliano ya muda mrefu ya viongozi wa Ukawa kuhusu Umoja wao, kulijitokeza mvutano wa kuachiana majimbo kadhaa, ambapo kila chama kilidai kinakubalika kwenye maeneo hayo na hivyo suala hilo kuachwa kulifanyiwa kazi kwa kina zaidi.
"Majimbo yote bado kufikiwa mwafaka wa pamoja na sasa tumepanga kukutana Aprili 28, mwaka huu Dar es Salaam kuweza kuweka wazi juu ya majimbo haya," alisema Profesa Lipumba.
Alisema kwa Jimbo la Morogoro Mjini pia bado maafikiano yanaendelea na kwamba moja ya sifa ni kuweka mgombea anayekubalika na wananchi wote.
Katika taarifa yake kwa umma hivi karibuni, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano,Tumaini Makene alisema Chadema na washirika wenzake wa UKAWA, bado wanaendelea na mazungumzo ya kusimamisha mgombea mmoja kwa nafasi za udiwani, uwakilishi, ubunge na urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mazungumzo bado yanaendelea vizuri, hayajafikia tamati na yakikamilika na makubaliano kufikiwa, viongozi wakuu wa UKAWA watatoa taarifa rasmi kwa umma wa Watanzania. CHANZO: HABARI LEO (Muro)

Mkosi wamwandama Brendan,Liverpool 

Kocha wa klabu ya Liverpool Brendan Rodgers yupo kwenye wakati mgumu baada ya kushindwa kutwaa taji lolote katika misimu mitatu ya mwanzo ya kuwanoa vijogoo hao wa Anfield.
Hii ni rekodi ambayo haijawahi tokea kwa kocha yeyote tangu mwaka 1950 ndani ya kikosi hicho. ,Je ni wachezaji wasiokidhi viwango?,au ni mbinu za kocha zilizogota mwisho?hayo ni baadhi ya maswali ambayo bado hayana majibu,huku Brendan Rodgers hata kama anakula basi chakula hakishuki uzuri kwani hajui nini hatima yake kufuatia kuboronga huko.CHANZO;BBC(V.S)

Anna Malecela atembelea Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Elimu...  


Naibu waziri Anne Kilango Malecela akiongea na wafanyakazi wa Mamlaka ya Elimu Tanzania(TEA) Jumatatu. Wa pili kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa TEA Bw. Joel Laurent, na watatu kutoka kushoto ni Bi, Paulina Mkoma kutoka wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Mhe. Anna Kilango Malecela ametembelea Mamlaka ya Elimu Tanzania katika ziara yake ya kutembelea Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. (Muro)

Mosri kuhukumiwa leo 


Mohamed Morsi
Mahakama nchini Misri inatarajiwa kutoa hukumu kwenye kesi kadha zinazomkabili rais wa zamani Mohammed Morsi ambaye aliondolewa madarakani na jeshi mwaka 2013.
Anakabuliwa na kesi pamoja na viangozi wengine wa kundi la Muslim Brotherhood kwa kuwachochea wafuasi kumuua mwandishi wa habari na waandamanaji wa upinzani wakati wa makabiliano nje ya ikulu ya rais mwaka 2012.
Mawakili wanamtetea bwana Mosri wamasema kuwa huenda akakabiliwa na hukumu ya kifo. Mamia ya wafuasi wa kundi la Muslim Brotherhood wamehukumiwa kifo katika mikakati ya kukabiliana na kundi hilo lililopiwa marufuku na rais wa sasa Abdul Fattah al-Sisi.
Kundi la Muslim Brotherhood limemlaumu rais kwa kutumia mahakama kama silaha.CHANZO:BBC (Muro)

Huenda 800 waliangamia baharini 


Mashua ya wahamiaji iliyozama.

Federica Mogherini
Umoja wa Mataifa unasema unahofia kuwa huenda watu 800 walifariki siku ya Jumapili, pale mashua waliyokuwa wakilitumia kuvuka bahari ya Mediterenean ilipozama karibu na Libya.
Shirika la Umoja wa mataifa linalowashughulikia wakimbizi UNHCR, limekuwa likizungumza na manusura baada ya kuwasili katika kisiwa cha Sicily mapema leo Jumanne.
Federica MogheriniMkuu wa sera kwenye Muungano wa Ulaya Federica Mogherini anasema kuwa pana haja ya kuwepo hatua za haraka ili kushughulikia suala kuhusu wahamiaji katika bahari ya Mediterranean, huku akizindua mikakati kumi ya mpango wa kutanzua vifo vya wahamiaji.
Mogherini, anasema kuwa mipango hiyo ni hatua kubwa ya kuzuia kupotea kwa maisha ya watu. Majukumu ya muungano huo ni kuzidisha operesheni ya uokozi, pamoja na mipango mipya ya kuharibu mashua zinazotumiwa na walanguzi wa binadamu wanaowavusha watu baharini.CHANZO:BBC (Muro)

Ulaya kumaliza vifo vya Wahamiaji? 


Picha za Kamera zikionyesha picha za baharini wakati wa Operesheni ya kuwaokoa wahamiaji
Mkuu wa sera za kigeni ndani ya Umoja wa Ulaya amesema kuwa uharaka unahitajika katika kushughulikia majanga yanayojitokeza katika bahari ya Mediterania.
Federica Mogherini ameainisha mambo tisa ya mpango wa kumaliza tatizo la vifo vya wahamiaji.
Operesheni ya uokoaji itaimarishwa na kutakuwa na Kampeni maalumu ya kuteketeza boti zilizotumiwa kusafirisha watu.
Waziri Mkuu wa Italia, Matteo Renzi, amesema Roma ina mpango wa kupambana na wale waliowaita Wafanyabiashara wa utumwa.
Imeelezwa kuwa hatua zitachukuliwa kupunguza idadi ya wahamiaji na kuwarejesha wale wanaoingia barani Ulaya.
Mpango huu utajadiliwa na Viongozi wa Ulaya siku ya Alhamisi.
Wakati hayo yakijiri,Polisi nchini Italia inawashikilia watu wawili miongoni mwa walionusurika kwenye ajali ya boti.
Mtu mmoja mwenye asili ya Tunisia ambaye anaaminika kuwa nahodha wa chombo hicho na mwenzake Raia wa Syria walikamatwa wakishukiwa kuhusika na vitendo vya kusafirisha watu kinyume cha sheria.
Watu hao walikamatwa baada ya meli moja yenye manusura wa ajali kuwasili katika bandari ya Catania katika kisiwa cha Sicily.BBC

Monday, April 20, 2015

Pembe za Ndovu zanaswa Thailand


Shehena ya pembe za Ndovu
Maafisa wakuu wa idara ya forodha nchini Thailand, wanasema kuwa wamenasa shehena kubwa zaidi ya pembe za ndovu kuwahi kunaswa katika historia ya taifa hilo.
Wanasema kuwa wamefuatilia chimbuko la shehena hiyo yenye uzito wa tani nne ya pembe za ndovu na kubaini zilitoka nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Maafisa hao wanasema kuwa pembe hiyo inayogharimu dola milioni sita ilikuwa njiani kwenda mjini Laos, ambako inaaminika ingeuzwa kwa wateja nchini Thailand, China au Vietnam.
Thailand inakabiliwa na vikwazo vya kiuchumi kuhusu namna inavyozembea katika kukabiliana na bidhaa za wanyama pori zinazouzwa nje ya Nchi hiyo, iwapo haitafanya lolote kuzuia biashara hiyo haramu ya pembe za ndovu.CHANZO:BBC (Muro)

Semina ya Texas Karate Black Belts yafanyika Houston, Texas 



Texas Black Belts club Seminar , imeandaliwa na Sensei Ramon Veras, Dan 7, Okinawa Goju Ryu Kyokai, mjini Houston, Texas tarehe 19 April, 2015. Pia ni sehemu moja ya maandalizi na marekebisho ya mbinu na ufundi wa vipande tofauti katika mfumo mzima wa Sanaa na tayari kwa baadhi ya washiriki kwa msafara wa kwenda kwenye chimbuko la Karate huko Okinawa, Japan.
Sensei Rumadha Fundi, ni mmoja ya wawakilishi wa Goju Ryu Jundokan, atayoiwakilisha Tanzania kwenye msafara huo..
Baada ya takriban miaka 23 sasa, sensei Rumadha Fundi "Romi", anarejea tena chini Japan kama alivyofanya mwezi May mwaka 1992. Safari hiyo ya mwezi June kwenda Naha City, Okinawa kwa njia ya Los Angeles, Tokyo na hatimaye Naha City, Okinawa.
Sensei Rumadha amepewa mwaliko kama mwakilishi wa Jundokan Tanzania, kwa niaba ya kuwa mteule na mwakilishi wa chama hicho cha mtindo wa Okinawa Goju Ryu, chini ya rais wake ambaye ni mtoto wa Eiichi Miyazato mwanzilishi wa chama hicho Sensei Yoshihiro Miyazato "Kancho", na hatimae kupewa jukumu la kusambaza Jundokan nchini kote akiwa"Tanzania Chief Instructor " na kupewa madaraka ya kutowa idhini na mikanda ya wawakilishi wa Jundokan nchini Tanzania na utambulisho wa kutowa vyeti ( Dan Certificate) kutoka, Naha, Okinawa.
Sensei Rumadha anashikilia Dan 6 toka Tanzania Karate-do Federation, na Dan 3 toka Jundokan Kyokai.Lengo na madhumuni ya sensei Rumadha ni kusambaza ufanisi wa Goju Ryu na mbinu za "Muchimi" ni undani halisi wa utumiaji mbinu kifasaha na kitamaduni kama ifanyavyo huko Okinawa, Japan.
Sensei Rumadha, atafanya mazoezi katika dojo ambayo mwalimu wake yeye Sensei Bomani na Master Morio Higaonna walikuwa wanafunzi hapo miaka 45-50 iliyopita. Pia Sensei Rumadha, atatembelea sehemu zenye historia ya mwanzao wa Karate na makaburi ya waanzilishi wa Sanaa na makumbusho ya Karate na vitongoji vyake kama, Naha, Shuri na Tomari, Okinawa , Japan.
Nia na madhumuni makubwa ni kutaka kuiendeleza Goju Ryu Karate Tanzania na hatimae kuwa na walimu wenye utambulisho huko, Okinawa, Japan na kuleta maendeleo na maslahi ya kimaisha kama mwalimu wa Karate.
Pia Sensei Rumadha alisema " Tapenda kubadilisha mfumo wa jinsi Goju Ryu inafundishwa Tanzania. Tawapa mwaliko wanafunzi wote wenye nia ya mafanikio na utambulisho toka Okinawa, kuwa chini ya uongozi wangu na kuendeleza utamaduni wa Goju Ryu. Goju Ryu ina matawi mengi na uongozi tofauti, mimi napendelea kuwa na shina la Okinawa Goju Ryu Karate – do, lililowekwa na waanzilishi wa mtindo huo; lengo ni kuwa na Goju Ryu halisi na sio mabadiliko", alisema Sensei Rumaha.(Muro)

Njia 3 muhimu katika ujenzi wa uchumi wa gesi Tanzania 

Ugunduzi huo mpya katika Kisima Piri-1 umefanyika katika eneo lenye kiwango kidogo cha mawe ya mchanga kama ilivyokuwa wakati ilipogunduliwa gesi katika Kisima cha Zafarani-1 mwaka 2012.PICHA|MAKTABA
Na Dk. A. Massawe
YA KWANZA
Mojawapo ya njia zitakazofanikisha matumizi ya gesi yetu asilia hapa chini yawe yenye tija zaidi ni ile ya kuisambaza maeneo yote nchini kwa kuanzia na miji mikuu ya kanda au mikoa kwa ajili ya matumizi ya majumbani na viwandani na kuzalisha umeme kwa ajili ya matumizi ya pale pale unapozalishwa.
Kusafirisha gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam itakakotumika kuzalishia umeme, majumbani na viwandani ni sahihi tu kama umeme wote utakaozalishwa utatumika ndani ya ukanda wa Dar es Salaam.
Yaani, ni sehemu kidogo tu ya gesi asilia inayowasili Dar es Salaam ingebaki hapo hapo kwa ajili ya kuzalisha umeme na matumizi ya majumbani na viwandani ndani ya ukanda wa Dar es Salaam na kitakachosalia kiendelee na safari yake hadi kanda nyingine za Tanzania kuzalisha umeme na kwa ajili ya matumizi mengine ya moja kwa moja majumbani na viwandani kuendana na mahitaji ya kila kanda.
Lengo ni kuondokana upotevu mkubwa wa umeme na gharama kubwa ya kuusafirisha umbali mkubwa kutoka kanda moja ya Tanzania hadi nyingine, pia ikizingatiwa kwamba, zaidi ya umeme, kila kanda hapa Tanzania pia inahitaji gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya moja kwa moja majumbani na viwandani kama Dar es Salaam.
Hivyo ni kosa kuzalisha umeme wa megawati 3000 hapa Dar es Salaam kutokana na gesi asilia ya Mtwara kwa ajili ya matumizi ya ukanda wa Dar es Salaam na kanda nyingine zilizoko mbali na Dar es Salaam kwani njia sahihi ni kusambaza uzalishaji wa umeme utokanao na gesi asilia kote nchini kwa kusambaza gesi asilia kote nchini kwa njia ya mabomba na kufunga mitambo midogo midogo ya uzalishaji wa umeme wa gesi asilia kwenye kila kanda kuendana na mahitaji halisi ya kanda.
Hivyo, cha muhimu zaidi kwenye kufanikisha matumizi ya gesi asilia hapa nchini yawe yenye tija tosha ni kujenga miundo mbinu ya mabomba kwa ajili ya usambazaji gesi asilia kikanda kote nchini itakakozalisha umeme na kutumika moja kwa moja majumbani na viwandani kikanda kuendana na mahitaji halisi kikanda ili kukwepa upotevu mkubwa wa umeme na gharama kubwa za kuusafirisha umbali mkubwa kutoka kanda hadi kanda, huku ikizingatiwa kwamba, zaidi ya umeme, kanda zote pia zinahitaji gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya moja kwa moja majumbani na viwandani kama Dar es Salaam.(P.T)
YA PILI
Njia ya pili itakayofanikisha matumizi yenye tija ya raslimali ya gesi asilia iliyogundulika hapa nchini ni kutumia hisa za Serikali kwenye raslimali hiyo iliyoko ardhini ikisubiria kuanza kuvunwa kama rehani kuchukulia mikopo kwa ajili ya ujenzi wa mitambo ya kuzalishia umeme wa maji huko Stigler's na wa makaa ya mawe huko Mchuchuma na kwingineko. Ni matumizi yanayowezesha kurudisha mikopo na kuleta faida hata kabla uchimbaji wa gesi asilia iliyotumiwa kama rehani haujaenda mbali sana, huku ikizingatiwa kwamba maelfu ya megwati za umeme wa maji ambazo hazijavunwa huko Stiglers na kwngineko hapa nchi huwa zikipotea kila saa miaka nenda rudi wakati gesi asilia na makaa ya mawe yanaweza kusubiri ardhini hadi uvunwaji wake kwa ajili ya uzalishaji wa umeme utakapoanza.
YA TATU
Njia ya tatu itakayofanikisha matumizi yenye tija tosha ya raslimali ya gesi asilia iliyogundulika hapa nchini ni kuwekeza mapato ya serikali yatokanayo na uvunwaji wa ralimali yake ya gesi asilia kwenye mfuko endelevu ''Sovereignity Fund''wa kutolea mikopo yenye riba nafuu kwa sekta za umma (kwa ajili ya kuwekeza kwenye ujenzi na uendelezaji wa miundo mbinu ya kitaifa na kwenye makampuni ya kimataifa yaliyo mihimili mikuu ya maendeleo ya uchumi wa dunia kisayansi na kiteknolojia (kuiwezesha Tanzania kuwa sehemu ya wahimili wakuu wa uchumi wa dunia kisayansi na kitknolojia na kuwa mmojawapo ya wanaonufaika sana), na kwa sekta binafsi (kuwezesha ukuwaji wa ujasiriamali hapa nchini).
Ni kuzingatia kwamba raslimali ya gesi asilia hapa nchini ni urithi usio endelevu wa vizazi vyote vya Tanzania, na njia ya kuhakikisha matumizi yake ni yenye manufaa makubwa zaidi kwa vizazi vyote vya Tanzania ni kutumia mapato ya serikali yatokanayo na uvunwaji wake kama kianzio endelevu cha mikopo yenye riba nafuu kwa sekta binafsi na za umma kote nchini.
Chanzo:wavuti.com

Sunday, April 19, 2015

Ndege ya kipekee inayotumia nguvu ya jua ilikwamia China, kitu kimoja tu kimeikwamisha (picha 10)

n13 
Ni ndege ambayo ilianza safari yake March 9 2015 Abu Dhabi na ikafanikisha salama safari zake kwa kupaa angani na kupita Oman, India na Myanmar.
Marubani wawili wanaoiendesha wanasema wanataka kuvunja rekodi kwa kuuthibitishia ulimwengu kwamba Ndege inayotumia nguvu ya Jua inaweza kutumika kwenye dunia ya sasa.
N1 
Pamoja na hayo, safari yao bado ni ndefu ambapo siku mbili zilizopita waliripotiwa na CNN kwamba safari yao imekwama China kwa zaidi ya wiki mbili baada ya kushindwa kupaa kutokana na hali mbaya ya hewa, hali ikiwa mbaya inavunja masharti ya kuipaisha ndege hii.
n2 
Jamaa wamepanga kuzunguka na hii ndege kwenye nchi mbalimbali za dunia lakini bila kutumia hata tone moja la mafuta, yani wanataka itumike nguvu ya jua kama ndege ilivyoundiwa.
N4
n5
n6
n7
n8
n9
n10
n11
n12

Mengine ya kujionea ndani na nje ya treni mpya ya Deluxe.. DAR-MWANZA ni poa kabisa yani

PIC 182
Labda umeyasoma yaliyoandikwa kuhusu uzuri wa treni ya Deluxe, hizi PICHAZ nilifikishiwa na ripota wangu nikaona nizisogeze hapa na wewe hata kama hautapanda hili ila uone tu mwonekano wa hii treni mpya ya Deluxe ambayo watu wetu wa Mwanza na Kigoma wanaenjoy sasa hivi kusafiri nayo.
PIC 180
Mwonekano wa nje
PIC 181
PIC 182
PIC 183
Mwonekano wa ndani ya mabehewa, siti zake ni kama umepanda kwenye basi
PIC 184
PIC 185
PIC 186
PIC 187
Huku ni jikoni, ndani ya treni hiyohiyo

Monday, April 13, 2015

African Sports yakwapua beki wa Simba kujipa makali 

AFRICAN Sports iliyopanda daraja kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao, imeanza usajili kwa kumnasa beki wa zamani wa Simba, Hassan Khatib na winga wa Kurugenzi ya Daraja la Kwanza, Jafar Kibaya.
Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja wa timu hiyo, Abdulhalim Hemed, alisema wapo kwenye hatua nzuri ya mazungumzo na wachezaji hao ambao wana sifa za mahitaji ya timu yao.
"Hao ni wachezaji kati ya watano ambao tuna uhakika wa kumalizana nao, kwani wengine tunaogopa kuwaweka wazi tunahofia hujuma za timu zenye fedha zao kwani wakisikia tu tunawasajili watataka wawasajili kwenye timu zao," alisema.(P.T)
Baada ya Khatibu kutemwa Simba , alijiunga na Friends Rangers ya Ligi Daraja la Kwanza , iliyopo chini ya katibu Herry Mzozo, anayeaminika kuibua wachezaji wengi wanaokipiga Ligi Kuu Bara, akiwemo Salum Abubakar 'Sure Boy' wa Azam FC.
Mbali na hilo alisema hawana mpango wa kuwasajili wachezaji wa Simba, Yanga na Azam FC kwa sababu hawataki ugomvi na timu hizo zenye sifa za kutumia fedha nyingi katika usajili isipokuwa wanaangazia macho yao katika timu ya Mtibwa Sugar.
"Hatuna haja na wachezaji wa Simba, Yanga na Azam FC, kwani timu yetu haina uwezo wa kushindana nao kifedha ili tutasajili wasio na majina makubwa, lakini wenye uchu wa mafanikio yao pamoja na timu kwa ujumla," alisema.
Mbali na hilo pia alisema wapo kwenye harakati ya kusaka wadhamini ambao ndio watakaowawezesha kukamilisha mpango wao wa usajili wa wachezaji ambao wamewaona ndio watakaoisaidia timu kufika pazuri.
"Kuna mambo mengi yanaendelea katika kikosi chetu ya kuhakikisha tunaanza ligi msimu ujao timu ikiwa imejipanga kwa ajili ya kufanya kazi na si vinginevyo," alisema.
http://www.mwanaspoti.co.tz/

JK awananga wanasiasa wanaotumia mgongo wa dini 


Rais Jakaya Kikwete akiwa kwenye picha ya pamoja na maaskofu wa kanisa la Katoliki mara baada ya kumalizika kwa ibada ya kumweka wakfu askofu mpya wa jimbo katoliki Shinyanga, Mhashamau baba Askofu Leberatus Sangu
Shinyanga. Rais Jakaya Kikwete amewataka viongozi wa dini nchini kutowaonea haya viongozi wa kisiasa wanaotaka kugeuza nyumba za ibada kuwa majukwaa ya kufanyia siasa kwa kuwa hali hiyo inaweza kusababisha vita ya kidini au waumini kwa waumini.
Rais Kikwete alisema hayo jana wakati wa ibada ya kuwekwa wakfu na kusimikwa rasmi, askofu mpya wa Jimbo la Shinyanga, Liberatus Sangu katika Kanisa la Mama Mwenye Huruma, Parokia ya Ngokolo, Shinyanga.
Aliwataka viongozi hao kuhakikisha makanisa na misikiti inabaki kuwa sehemu ya ibada na usuluhishi na iwapo watashindwa, inaweza kusababisha makundi na mapigano.
"Katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, wanasiasa wengi wanapenda kutumia tofauti za rangi, ukabila na dini nawaomba msiruhusu mambo hayo ni hatari kwa Taifa, endeleeni kukemea jambo lolote ambalo mnaona linakwenda tofauti."
Rais Kikwete pia alizungumzia mauaji ya vikongwe na albino huku alimtaka Askofu Sangu na maaskofu wengine kuongeza bidii kuwalea waumini wao katika imani, ili waachane na vitendo vya kishirikina ambavyo ndivyo chanzo cha mauaji yao.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Muadhama Polycarp Kardinali Pengo alimsimika rasmi Askofu Sangu na kumkabidhi fimbo ya kichungaji huku akimtaka kuhakikisha anafanya kazi kwa kushirikiana na viongozi wengine na kumtakia heri na baraka katika muda wake wote wa kitume.
Kwa upande wake, Askofu Sangu alisema kazi kubwa iliyo mbele yake ni kuhakikisha analinda na kustawisha mema yote yaliyoachwa na waliomtangulia.
"Nitashirikiana na viongozi wenzangu pamoja na Serikali katika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukemea mauaji ya vikongwe na albino. Sala zenu ndizo ambazo zimesababisha mimi nikateuliwa na baba mtakatifu kuwa askofu na leo hii nimesimikwa rasmi kuanza kazi katika jimbo hili la Shinyanga, nawaomba waumini wote tushirikiane kwa pamoja katika kazi hii."
Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa alimtaka Askofu Sangu kuchunga kondoo wake aliokabidhiwa kwani wanahitaji upendo pamoja na kushirikiana vizuri na wasaidizi wake katika kuleta maendeleo na kuwalea waumini kiimani.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwamo waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa.CHANZO: MWANANCHI (Muro)