TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Sunday, May 18, 2014

‘KUNA DALILI BUNGE LA KATIBA LITAPORA MAMLAKA YA WANANCHI

bu_2adac.jpg
Bunge la Katiba limesitishwa kwa muda baada ya kukutana kwa takribani miezi miwili na nusu na kufanya mijadala muhimu inayolenga kuboresha rasimu ya katiba.
Mjadala wa Rasimu ya Katiba hiyo yenye ibara 271 na viambatanisho vinane limetawaliwa na changamoto nyingi, ikiwemo baadhi ya wajumbe kutoka Kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kujitoa.
Kujitoa kwa Ukawa kumedaiwa kutokana na kupinga mwenendo wa bunge hilo, kutawaliwa na matusi, vitisho, kashfa, ubaguzi na pia kuwekwa pembeni Rasimu ya Pili ya Katiba iliyowasilishwa katika bunge hilo na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Mwenendo wa bunge hilo, sasa umeziamsha Asasi za Kiraia (Azaki) zaidi ya 1,000 na kuamua kutoa tathmini ya mwenendo wa bunge hilo.
Mwenyekiti wa Azaki katika masuala ya Katiba, Irinei Kiria na katibu wake, Onesmo Ole Ngurumwa katika tathmini ya umoja huo, wanaeleza kutoridhishwa na mwenendo wa Bunge la Katiba.
Ole Ngurumwa ambaye ni Mkurugenzi wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za binadamu (THRDC) kwa niaba ya Azaki anazungumza na gazeti hili na kufafanua msimamo wa Azaki unaotokana tathmini ya Mchakato wa Katiba na kuangalia tulikotoka, tulipofikia na tunakoenda.
"Tathmini ya Azaki imejikita katika kuangalia zaidi Mwenendo wa Mchakato wa Katiba hasa hatua ya sasa ya mjadala katika Bunge la Katiba na pia hatua inayofuata ya kupitisha katiba pendekezwa kwa njia ya kura ya maoni," anasema Ole Ngurumwa.
Anafafanua kuwa, mwenendo wa sasa wa Bunge la Katiba umelenga kutoa msimamo wa Azaki katika Mchakato wa Katiba, kushauri na kukemea yale ambayo yanayoweza kuwakosesha Watanzania fursa ya kupata katiba waitakayo na kwa muda mwafaka.
"Tunafahamu kabisa katiba yoyote ile ni lazima ipate uhalali kwa makundi yote katika taifa ili iweze kutekelezeka na njia nzuri ya kupata katiba itakayokuwa na sura ya kitaifa ni kuandaa sheria na taratibu shirikishi na kuziheshimu"anasema Ole Ngurumwa.
Anaeleza kuwa ni muhimu sana, wajumbe wa Bunge la Katiba. kuheshimu ngazi zote za kisheria katika mchakato pamoja na kuzingatia suala la maridhiano ni njia nzuri ya kupata katiba yenye ridhaa ya wananchi wote.
Msimamo wa Azaki
Ole Ngurumwa anasema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ndiyo inatumika sasa Ibara ya 8(1) (a) wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi
Anaeleza kuwa tofauti na michakato yote ya kupata katiba iliyokwishafanyika miaka ya nyuma, mchakato wa sasa ni wa kwanza na wa kipekee ambao umetambua na kuyatafuta maoni ya wananchi katika kupata katiba ya nchi yao.
"Kimsingi mchakato huu ambao ni mwitikio wa madai ya wananchi kwa miaka mingi na kuanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano Jakaya Kikwete unakidhi matakwa ya Hati ya Makubaliano ya Muungano kama inavyojieleza katika ibara yake ya saba," anasema Ole Ngurumwa.
Ole Ngurumwa anasema Azaki zinaamini kuwa, katika mchakato huu, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilikusanya na kuchambua maoni ya wananchi ambayo yametoa taswira ya kile ambacho wananchi wamesema wanakitaka.
Kwa nini wanatetea Rasimu ya Pili
Ole Ngurumwa anasema Azaki zinatetea Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kwani hadi sasa hakuna maoni yoyote ambayo kisheria yanapaswa kufanyiwa kazi na Bunge la Katiba zaidi ya yale yaliyomo kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba.
"Kwa kuwa wananchi waliotoa maoni ndio msingi na chimbuko la madaraka yote na mamlaka ya nchi na ni kwa kupitia rasimu hii wananchi wametamka Muundo wa Uongozi namna ya kuwapata na kuwawajibisha viongozi na wamegawanya madaraka kwa viongozi wao," anasema Ole Ngurumwa.
Haturidhishwi na mwenendo wa Bunge
Ole Ngurumwa anasema Azaki, zinaamini kuwa majadiliamo bungeni yamekosa utashi wa utaifa kutokana na baadhi ya wajumbe kupoteza moyo wa maridhiano na kuheshiminiana. Ole Ngurumwa anasema Mwenendo mzima wa Bunge Maalumu la Katiba kuchukua sura ya ubinafsi na yenye maslahi ya kivyama zaidi na kusahau masilahi ya Watanzania na mustakabali wa Taifa.
Anasema mwenendo wa kusuasua unaotia shaka unaonesha kuwa wapo Watanzania wenzetu wasio na nia njema ya kufanikisha katiba mpya kwa muda muafaka na hivyo ucheleweshaji wa makusudi unalenga kufanikisha malengo hayo.
Katibu huyu anafafanua kuwa, wamebaini uwepo wa mazingira na kila dalili ya kutaka kulipa Bunge la Katiba madaraka makubwa yasiyostahili ya kutupilia mbali rasimu hii ya wananchi na kuja na rasimu inayopendekezwa na watawala.
Anasema Azaki haziridhishwi na lugha ya vitisho na ubaguzi kwa wananchi na hata kwa wajumbe wa Bunge la Katiba wenye misimamo huru na hasa kwa wale wanaosimama na kutetea maoni ya wananchi.
"Vitisho hivi ni pamoja na kauli ya Rais Jakaya Kikwete na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu, William Lukuvi kuwa muundo wa serikali tatu, unaweza kutoa mwanya kwa jeshi litapindua nchi, "anasema
Wito
Anasema kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83 Toleo la 2014, kifungu cha 27(2), Bunge la Katiba na wajumbe wake wanapaswa kuwa huru katika kujadili na kupendekeza katiba mpya.
"Ni muhimu tutambue kuwa kati ya wananchi milioni 45, wenye itikadi za vyama hawafiki milioni saba, hivyo ni kosa kubwa kugeuza mjadala wa Bunge la Katiba kuwa Uaja wa siasa za vyama badala ya kujadili Katiba," anasema.
Anasema bunge halina mamlaka ya kubadili mambo ya msingi ya katika Rasimu ya Katiba. "Bunge linakosa uhalali huo kwanza kutokana na muundo wa mchakato wa uandaaji wa Katiba hapa nchini. Muundo wetu umekuwa shirikishi na kuundwa kwa tume kwa ajili ya kukusanya maoni ya wananchi tayari kumelipunguzia Bunge madaraka makubwa," anasema.
Anasema kwa maana hiyo Bunge hili halina mamlaka ya kubadili rasimu hii zaidi ya kujadili, kuboresha na kuongeza masharti ya mpito. Pili, Kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 imeweka bayana kuwa Bunge lina madaraka tu ya kujadili na kupitisha masharti ya katiba, .(E.L)

5 WAUAWA KATIKA MLIPUKO NIGERIA

n_f49c9.jpg
Bomu lililolipuka katika mji wa Kano kaskazini mwa Nigeria limewaua watu 5 na kuwajeruhi wengine wengi.
Shambulio hilo limefanywa katika eneo linaloaminiwa kuwa na waumini wengi zaidi wa dini ya kikristu, ambao wamekuwa wakilengwa mara nyingi na wapiganaji wa Boko Haram.
Mwandishi wa BBC mjini Abuja Will Ross anasema kuwa eneo hilo lililolengwa linajulikana kama Sabon Gari. Watu wengi walikuwa kwenye migahawa ya vileo na kwenye barabara. Amesema kuwa kilichosalia kwenye gari lililokuwa na bomu hiyo ni injini pekee.
Kwa zaidi ya mwaka mmoja mji wa Kano umepumzika kutokana na mashambulio, hasa kwasababu ya oparesheni kali iliyofanywa na maafisa wa usalama kuwasaka wanamgambo hao wa Boko Haram.
Mashambulio ya awali
Mnamo mwezi Machi mwaka uliopita kituo cha basi kilishambuliwa kwa bomu na awali mwaka wa 2012, Boko Haram walifanya shambulio baya zaidi lililowaua zaidi ya watu 150 katika msururu wa milipuko.
Kundi hilo bado linawazuilia wasichana zaidi ya 200 wa shule, lililowateka kutoka kijiji kimoja kaskazini mashariki mwa Nigeria mwezi mmoja uliopita.
Nchi kadhaa zikiwemo Uingereza, Ufaransa na Marekani wameahidi kutuma wanajeshi kusaidia kuwakomboa wasichana hao.
Nao viongozi wa Afrika wanaokutana mjini Paris wametangaza 'vita' dhidi ya Boko Haram na kuahidi kushirikiana ki-intelijensia na kijeshi, kupambana na Boko Haram.(E.L)

UTALII WA NGONO WANAWIRI MALINDI KENYA


Utalii wa Ngono wanawiri Malindi Kenya

Unapouzuru mji wa Malindi uliopo kwenye mwambao wa Kenya unaonekana kama paradiso.
Hata hivyo mji huu ni kitovu kilichojificha cha biashara ya ngono ya watoto .

Watoto wadogo wenye umri wa miaka hata 12 hutumiwa katika ukahaba na filamu za ngono na watalii ambao huwa tayari kulipa pesa nyingi kwa ajili ya ngono katika maeneo yaliyojificha .
Maafisa wanasema biashara hii imependwa sana na wasichana hao wadogo na wavulana kiasi kwamba wengi wao huacha shule .
Kijana mmoja mwenye umri wa miaka kumi na saba ameiambia BBC kuwa aliacha shule kutokana na ufukara.
Alivutiwa kuingia katika biashara ya ngono baada ya rafiki yake aliyekuwa akifanya kazi hiyo kukutana na mtalii aliyempeleka bara Uropa na sasa anaishi maisha ya ustaarabu.
Maisha ni hayo hayo pia kwa wasichana.

Utalii wa Ngono wanawiri Malindi Kenya
Msichana mmoja ameiambia BBC kuwa alianza biashara ya ngono akiwa na miaka 15, bila mamake kujua.
Anaeleza ugumu wa biashara hiyo na jinsi wasichana wanavyogeuzwa kuwa watumwa wa ngono na hata kulazimishwa kushiriki tendo hilo na wanyama kama mbwa.
Hatahivyo anasema haoini ubaya wowote kwani ndiyo njia pekee inayomuwezesha kujimudu kimaisha.
Juhudi za mamake kumshawishi aiache biashara hiyo zimeambulia patupu.
Ni suala linalowasumbua viongozi katika jamii hii. Naibu chifu wa kata ndogo ya Shela, Mayele anasema watu wengi hawatoi ripoti kwa serikali.
Sasa Chifu huyo ameanzisha harakati kwa jina ''rudi shule'' ambapo watoto wakipatikana mjini wakati wa shule wanakamatwa na kupelekwa nyumbani, kisha wazazi wao kukamatwa na kufunguliwa mashtaka.
Anaamini kwamba mambo yataimarika, lakini changamoto bado ni nyingi.

BONDIA COSMAS CHEKA AHAIDI KUTETEA TAJI LAKE VIZURI 


Cosmas Cheka 'kulia'

Na Mwandishi Wetu
BONDIA Cosmas Cheka anatarajia kupanda ulingoni Juni Mosi kwa ajili ya kutetea taji lake la ubingwa wa TPBO anaoshikilia kwa kupambana na Suma Ninja katika ukumbi wa vijana socil hall  wa Morogoro.
Akizungumzia mpambano huo Cheka amesema amejiandaa kupigana kawa raundi kumi hivyo mashabiki waje kuona kazi anayoifanya akiwa ulingoni bondia huoyo ambaye anatamba sambamba na kaka yake Fransic Cheka ambaye alikuwa bingwa wa WBF ambao alivuliwa kizembe amesema yeye anataka afike mbali zaidi ya kaka yake huyo.
Mpambano huo utakaosimamiwa na TPBO utasindikizwa na mapambano ya utangulizi kati ya Kudura Tamimu atakae vaana na Sadiki Yusufu wakati Mohamed Matimbwa ataoneshana umwamba na Twaha Kassimu 
Siku hiyo kutakuwa pia na huzwaji wa DVD kali za ngumi wakiwemo mabondia wakali wanaotamba Duniani na hapa nchini kama Mohamed Matumla vs Fransic Miyeyusho,Japhert Kaseba Vs Thomas Mashali .Floyd Mayweathar,Manny Paquaio, Saul 'canelo' alverez, Mike Tyson, Mohamed Ali, Ferex Trinidad, Miguel Cotto na wengine wengi.
DVD hizo za ngumi kali zitakuwa zikiuzwa na kocha wa kimataifa wa mchezo wa masumbwi nchini Rajabu Mhamila 'Super D.'
Pamoja na kutambua sheria na taratibu za mchezo huo siku hiyo pia kuta kuwa na vifaa vya mchezo huo wa masumbwi vitakavyotolewa  zawadi kwa mabondia na Kocha Super D  ambaye ame haidi kutoa, Gum Shit ,Clip Bandeji,DVD za Mafunzo kwa mabondia, Bukta,Protector na vifaa mbalimbali kwa mabondia watakao onesha uwezo wa ali ya juu wa kutupiana masumbwi.

JAJI WARIOBA:VIONGOZI WATOA MATUSI WANA MATATIZO YA MAADILI 

w_83730.jpg
"Katika hali ya kawaida kiongozi anatarajiwa kuwa mfano kwa kutenda sawa kimila, kidesturi na kisheria lakini ninashangaa kushuhudia kiongozi akitoa lugha zisizofaa na hata matusi, ni ishara ya mmomonyoko wa maadili kwa kiwango kisichomithilika."
Siyo kauli yangu, ni kauli ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Waziri Mkuu mstaafu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu na Jaji Joseph Sinde Warioba, akizungumzia utendaji wa Bunge Maalumu.
Amezungumza hayo kupitia kituo cha televisheni cha ITV, kwenye kipindi cha dakika 45 ambacho hutangazwa mara moja kwa wiki.
Wakati hali ikiwa hivyo, Jaji Warioba anasema haelewi lengo la viongozi wa kisiasa wanaopinga mapendekezo yaliyo kwenye rasimu, yanayotaka Katiba ijayo iwe na mwongozo juu ya maadili ya viongozi.
"Hawataki mambo ya maadili ya viongozi yawe kwenye Katiba, wanataka yabaki kwenye sheria hata Uwazi na Uwajibikaji ambazo zimependekezwa kuwa Tunu za taifa kwakuwa ni msingi wa maadili ya viongozi, zinapingwa," anaeleza Jaji Warioba Ingawa anasema hana tatizo na uamuzi wa kuondoa au kuongeza mambo kwenye rasimu, Jaji Warioba anasema haitakuwa sahihi kuondoa matakwa ya msingi ya wananchi.
Anasema kupitia kukusanya maoni kutoka kwa wananchi, wamebaini malalamiko na matarajio mengi ya wananchi yanatokana na kukosekana msingi wa maadili ya viongozi, kwenye Katiba.
Anasema Watanzania wengi wamekata tamaa kutokana na kukithiri vitendo vya rushwa, huduma duni za kijamii na umaskini akisema ufumbuzi wa hayo ni kudhibiti maadili ya viongozi.
Jaji Warioba anasema wapo wanaopinga hata kuwapo ukomo wa kugombea ubunge, hali anayoamini siyo sahihi.
Rais Jakaya Kikwete, akitoa hotuba siku chache baada ya rasimu kuwasilishwa bungeni, akaagiza pendekezo la ubunge kuwekewa ukomo liangaliwe upya na Bunge Maalumu.
"Jiridhisheni na dhana zilizoingizwa, mtakachoona kinafaa kurekebishwa, kuboreshwa au kufutwa msisite tunataka Katiba bora, tofauti yake itapatikana Katiba isiyotekelezeka na kusababisha ilazimike kubadilishwa muda mfupi baadaye," anaeleza na kuendelea.
"Rasimu ina mambo mengi mapya, yatakayobadili mfumo wa utendaji wa nchi, jiridhisheni neno kwa neno, mstari kwa mstari."
Akatoa mfano wa Ibara ya 128.-(2)(d) ya rasimu, sababu za mtu kukoma kuwa Mbunge (d) ikiwa atashindwa kufanya kazi za mbunge kwa muda wa miezi sita mfululizo, kutokana na maradhi au kizuizi ndani ya gereza. Rais Kikwete anasema tatizo halitakiwi kuwa kizuizini bali kupatikana na hatia. Hata hivyo akasema, "Watu wanasema siyo mimi" Bila kuwataja, akasema watu hao wanasema anachositahili mgonjwa ni huduma.
Hoja hapa ni je, kuna ajira ambayo mwajiriwa asipofanya kazi kwa muda huo, kutokana na sababu yoyote zikiwamo zilizotajwa anabaki kwenye ajira? kama haipo, kwa Mbunge.
Rais anatoa mfano wa Ibara ya 125(2)(a) akitaka Wajumbe waiangalie. Inasema; Mtu hatakuwa na sifa za kugombea ubunge ikiwa, (a) aliwahi kuwa Mbunge kwa vipindi vitatu vya miaka mitano.
"Aliyewahi kuwa mbunge kwa awamu tatu eti hatakuwa mbunge milele, duniani kote hawaweki ukomo kwa ubunge hili likipita, tutakuwa wa kwanza," anaeleza Rais Kikwete.
Rais Kikwete anasema watu hao wanatoa mfano wa USA (nchi ya Marekani) kwamba baadhi ya majimbo yameweka ukomo wa kugombea ubunge, lakini wanasumbuana mahakamani kila mara kwa madai ya haki za binadamu kukiukwa."
Akitoa semina kwa Wajumbe wa Bunge hilo, mtaalamu mbobezi wa sheria nchini Kenya, Seneta wa Busia ya Mashariki, Amos Wako, alisema kujifunza kwa nchi nyingine ni vizuri lakini ni kunakiri kitu bila kuzingatia matakwa ya jamii inayolengwa ni hatari.
Seneta Wako aliyeulizwa maswali 40 na wajumbe 16, hakujibu wali hata moja lililolenga kupata ushauri dhidi ya changamoto za mchakato wa Katiba Mpya, alielezwa wazi kuwa majibu ya changamoto hizo yanatakiwa kutolewa na Watanzania wenyewe.
Jaji Warioba ataka wajumbe waweke kando itikadi zao za kisiasa na makundi mengine, ili watumikia taifa. Anabainisha cha msimamo wao wa kusimamia utaifa.(E.L)

Saturday, May 17, 2014

Mwanamke aliehukumiwa kifo kwa kubadili dini na kuolewa na mume Mkristo

Screen Shot 2014-05-16 at 12.52.30 PM 
Mahakama nchini Sudan imemuhukumu kifo mwanamke mmoja anayedaiwa kubadili dini yake na kuolewa na mwanaume mkristo.
Daktari Mariam Yahya Ibrahim Ishag ambae baba yake ni muisilamu alishitakiwa kwa kosa la kuasi dini pamoja na kufanya zinaa kwa kuolewa na mwanamume mkristo kitu ambacho dini ya kiisilamu imeharamisha kwa Wanawake.
BBC wamesema Mariam mwenye umri wa miaka 28 pia ni mjamzito na ataadhabiwa kwa kuchapwa mijeledi miamoja kwa kosa la zinaa.
Unaambiwa Mariam alilelewa na mama yake mzazi ambae ni Mkristo lakini maafisa wa Sudan wanasema yeye bado ni Muislamu kwa sababu ndio dini ya baba.

Alipewa siku tatu baada ya kuhukumiwa aweze kurejea katika dini ya kiisilamu lakini akakataa na ndio maana adhabu ikabaki palepale kwa kuwa Wanawake Waislamu hawaruhusiwi kuolewa na Wanaume Wakristo ingawa Wanaume Waisilamu wanaruhusiwa kuwaoa wanawake wakristo.
Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty International linasema kuwa Ishag alilelewa kama Mkristo muorthodoxi kwa sababu baba yake hakuwepo naye maishani mwake.
Kesi ya Ibrahim ni ya kwanza ya aina yake kusikika nchini Sudan kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters na Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu, wamelaani uamuzi huo wa Mahakama na kuitaka serikali ya Sudan kuheshimu haki na uhuru wa watu kuabudu.
Maafisa wa balozi za mataifa ya magharibi pia wamekemea vikali kesi hiyo na kuelezea asiwasi wao na kuwataka maafisa wa sheria nchini humo kuangalia kesi hiyo upya na kuhakikisha kuwa Mariam anatendewa haki.
Waziri wa mawasiliano amesema kuwa sio Sudan peke yake ambako sheria za kiisilamu zinafuatwa na ambako sio sawa kwa mtu kubadili dini yake, hali hiyo pia ipo nchini Saudi Arabia na katika nchi nyngine zinazofata sheria za kiisilamu.
Serikali ya Rais Omar al-Bashir inakabiliwa na changamoto nyingi za kiuchumi na kisiasa hasa baada ya kujitenga na Sudan Kusini ambako mafuta yake yalikuwa yanatoka mwaka 2011.

Mbali na kufeli kwa msimu uliopita,hii ndiyo faida waliyopata Manchester United.

man u
Kwa mfatiliaji yoyote wa mpira wa miguu ligi ya England Manchester United ni timu ambayo haikufanya vizuri makombe yote ya msimu uliopita kitu ambacho kimekua tofauti kwa timu hiyo.
Kwenye kipindi cha miezi mitatu ya mwisho wa msimu huu Man United walipata faida ya pauni milioni 11 ikilinganishwa pauni milioni 3.6m ambazo walipata mwaka uliopita na katika msimu huo Manchester United imeripoti faida ya asilimia 20 katika kipindi cha msimu huu ambao haikufanya vizuri.
Aidha timu hiyo ilipata jumla ya pauni milioni 115.5 katika msimu uliopita ambapo asilimia kubwa ya faida hiyo ilipatikana kutoka kwa mauzo haki ya upeperushaji matangazo na mapato kutokana na tiketi za mechi.
Taarifa iliyopo ni kwamba Man United inasemekana imesaini mkataba wa miaka mitatu na kocha wa Uholanzi Louis van Gaal ambaye ndiye atakua mrithi wa David Moyes,aliyefukuzwa kazi mwezi uliyopita baada ya matokeo mabovu ya timu hizo.
Mapato yaliyotokana na hati ya upeperushaji wa mechi za timu hiyo yaliimarika kwa asilimia 64 ama pauni milioni 35.6m ilihali faida iliyotokana na uuzaji wa tiketi za mechi ilileta pauni milioni £37.1m.
Kutokana na faida hiyo kubwa Manchester united imepunguza deni lake kwa takriban pauni milioni 16 na sasa deni lililosalia ni pauni milioni £351.7m.
Kulingana na kampuni ya uhasibu ya Deloitte Football Money League, Manchester United inaorodheshwa ya nne bora miongoni mwa vilabu tajiri zaidi duniani.
Hisa za klabu hiyo ya Manchester United zilianza kuuzwa kwenye soko la hisa la New York Stock Exchange mwaka wa 2012 .

Yule mfanyakazi aliyetoa video ya Jay Z akipigwa na Solange amefukuzwa kazi

Screen-Shot-2014-05-12-at-10.22.51-PM
Inasemekana yule mfanyakazi ambaye aliitoa ile video inayomuonyesha rapa Jay Z akishambuliwa na shemeji yake Solange Knowles ndani ya lifti ya hotel hiyo amefukuzwa kazi.
Katika video hiyo siku hiyo Solange Knowles ameonekana kuwa na hasira mno huku akimshambulia Jay Z,ingawa mpaka sasa haijafahamika nini kilichosababisha hali hiyo kwenye lift,video ambayo ilitolewa kwa mara ya kwanza kwenye tovuti ya watu maarufu TMZ, ilimwonyesha Solange Knowles ambaye ni dadake Beyonce akimpiga Jay Z baada ya tamasha la Met lililofanyika Los Angeles Mei 5.
Baada ya ugomvi huo kwenye video mlinzi anaonekana akiingilia kati akisuluhisha ugomvi huo hata hivyo video hiyo haina sauti,Hoteli The Standard imesema kuwa ilishtushwa sana na kutolewa kwa video hiyo ambayo hukusanya matukio ya kwenye lift..
Mfanyikazi huyo amefukuzwa kazi kwa kosa la kuvunja sheria za usalama kwa kutoa video za CCTV ambazo huwa ni za siri.
Hii ndiyo hiyo video inayomuonyesha Jay Z akishambuliwa na shemeji yake.

Wednesday, May 14, 2014

UNDP KUIWEZESHA TUME YA UCHAGUZI 


Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo (UNDP), Hellen Clark akikabidhi moja ya kompyuta mpakato kati ya 60 kwa mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damiani Luvuva, alipokutana na wakuu wa NEC, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) pamoja na mabalozi wa nchi mbali mbali za Ulaya, Dar es Salaam jana. Kulia ni Mkurugenzi wa Uchaguzi kutoka NEC, Julius Malaba. Picha na Emmanuel Herman. (J M)
Dar es Salaam. Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limeeleza nia ya kuisaidia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili ifanikishe matumizi ya mashine za kisasa za Biometric Voters Register (BVR) wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
Mkurugenzi wa shirika hilo, Hellen Clark alitoa ahadi hiyo jana na kuongeza kuwa hata hivyo, matumizi ya mashine hizo yamechelewa kwani zilitakiwa zitumike tangu uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, muda uliobaki unahitaji utekelezaji ili zitumike mwakani.
Clark ambaye pia ni waziri mkuu wa zamani wa New Zealand, alisema hayo wakati akizungumza na wanahabari kuhusu ziara yake ya siku nne nchini.
Alisema alipokuja nchini mwaka 2010 alitembelea NEC na kuziona kompyuta zilizokuwa zikitumika kusajili wapigakura kuwa zilikuwa zinatumia mfumo uliopitwa na wakati.
“Natambua kuwa kuna mpango wa kuwenda kwenye mashine za BVR ambazo zitahusisha uchukuaji wa alama za vidole na mambo mengine, natambua kuwa uamuzi umeshachukuliwa kuhusu mfumo huo, umechelewa, lakini sasa utekelezaji unatakiwa,” alisema.
Kauli hiyo imetolewa siku chache baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kulitaarifu Bunge mjini Dodoma kuwa NEC inaendelea na maandalizi ya kupata vifaa vya kisasa kwa ajili ya zoezi la kuboresha daftari la kudumu la wapigakura.
Pinda alitoa kauli hiyo wakati alipokuwa akisoma hotuba kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya matumizi ya fedha ya ofisi yake na ofisi ya bunge kwa mwaka 2014/15.
Katika hotuba yake, Pinda alieleza kuwa mfumo wa BVR utakaotumika ni tofauti na mfumo wa awali wa Optical Mark Recognition (OMR) ambao ulikabiliwa na changamoto nyingi za utendaji.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Damian Lubuva akizungumza na gazeti hili hivi karibuni, alisema kuwa mashine za BVR zitatumika wakati wa uandikishaji wapigakura pekee yake.
Akizungumza kwa kujiamini, Hellen alisema Tanzania imeshafanya uchaguzi mara nne kwa mafanikio makubwa.
Alisisitiza kuwa UNDP ipo tayari kutoa msaada wowote wa kiufundi ingawa mpango huo ni wa kitaifa, lakini mradi wa wa shirika hilo unatoa nafasi kuisaidia NEC.
Clark ambaye ameshafanya ziara nne nchini, alisema kuwa wadau mbalimbali wanaoshirikiana na shirika lake wameshatoa dola 22 milioni sawa na Sh35.2 bilioni kusaidia mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani.
“Hali kadhalika, tutashirikiana nanyi katika kuhakikisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wanashiriki kwenye uchaguzi huo,” aliongeza.
Hata hivyo, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe wakati akiwasilisha taarifa ya kambi yake bungeni kwenye Bunge la bajeti mwaka jana, alimtaka Waziri Mkuu Pinda kuiamuru NEC kusimamisha maandalizi ya mfumo wa uchaguzi wa elektroniki hadi hapo itakapowashirikisha wadau.
Mbowe alisema tayari NEC imekiri kuanza maandalizi huku wadau wa uchaguzi vikiwamo vyama vya siasa hawajashirikishwa.
Ujangili Tanzania
Akieleza masuala aliyozungumza na Rais Jakaya Kikwete, Clark alisema kuwa alimwelezea changamoto za ujangili na umaskini aliouona alipotembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, kwamba kuna umaskini mkubwa, njaa, watoto hawapati elimu ya kutosha na kinamama wajawazito wanakufa kwa sababu zinazoweza kuzuilika.
CHANZO, MWANANCHI

DK SHEIN AKATAA KUONGEZA POSHO BLW


Dk Shein amewataka wajumbe kuwa na subira kwa kipindi hiki hadi hali itakaporuhusu kiuchumi na suala hilo linaweza kufikiriwa.PICHA|MAKTABA.
 Zanzibar. Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amekataa maombi ya kuwaongezea posho wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW) kutoka Sh150,000 hadi Sh200,000. (J M)
Uamuzi huo wa Dk Shein umetokana na hali ya uchumi Zanzibar kutoruhusu nyongeza hiyo kwa sasa.
Katibu wa BLW, Yahya Khamisi Hamad alithibitisha jana kuwa baraza hilo lilipeleka kwa Rais Shein maombi la kutaka posho ya vikao hivyo iangaliwe upya kutokana na sababu mbalimbali, lakini kulingana na mazingira ya hali ya uchumi ilivyo kwa wakati huu imeshindikana kufanya hivyo.
Hamad alisema Dk Shein amewataka wajumbe kuwa na subira kwa kipindi hiki hadi hali itakaporuhusu kiuchumi na suala hilo linaweza kufikiriwa.
Alisema Dk Shein alitoa msimamo huo alipokutana na Spika wa baraza hilo, Pandu Ameir Kificho kwa nia ya kumweleza uamuzi kuhusu suala hilo. “Rais amekataa maombi ya nyongeza ya posho za vikao vya wajumbe wa BLW kutokana na hali ya mazingira ya kiuchumi kutokuwa mazuri kwa wakati huu, amewataka wawe na subira hadi hali ya mambo itakapotengamaa,” alisema Hamad.
Alisema kamati ya uongozi ya baraza hilo tayari imekwishataarifiwa kuhusu maombi ya posho kukataliwa na wajumbe wote kutoka CCM na CUF walitarajiwa kutaarifiwa jana kuhusu uamuzi huo.
Wajumbe hao wamekuwa wakilipwa posho ya Sh 150,000 kwa siku mbali na mshahara na posho nyingine zinazokaribia Sh4,500,000 kwa mwezi.
Akizungumzia kikao cha bajeti kinachoanza leo mjini Zanzibar, Hamad alisema kikao hicho kitalazimika kupunguzwa kwa siku ili kuwahi Bunge Maalumu la Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linalofanyika Dodoma ambalo lipo likizo na linatarajiwa kukutana Agosti 5.
Alisema kwa mujibu wa ratiba, kikao cha bajeti kinatarajia kutumia siku 56, tofauti na miaka mingine ili kukimbizana na muda na kuwataka wajumbe kujadili bajeti ili kuokoa muda na kuwahi Bunge la Katiba.
Aidha, katibu huyo wa BLW alisema kikao hicho kitakuwa na maswali 90, miswada miwili ya sheria ukiwamo wa Sheria ya Fedha na ule wa Sheria ya Kuidhinisha Matumizi ya Serikali mwaka 2014/2015.
Tayari, Waziri wa Fedha, Omar Yussuf Mzee amesema SMZ katika mwaka huu wa fedha inatarajia kutumia Sh 705.1 bilioni, kati ya hizo, makusanyo ya Serikali yatakuwa ni Sh 399 bilioni na kiasi kingine cha Sh 305.3 bilioni ni misaada ya wahisani na mikopo mbalimbali.
CHANZO, MWANANCHI

WACHIMBA MGODI 200 WAFARIKI UTURUKI 


57 wameaga dunia katika mkasa wa moto ndani ya mgodiMlipuko katika mgodi wa makaa ya mawe magharibi mwa Uturuki umesababisha vifo vya zaidi ya wachimbaji migodi 200 na kujeruhi wengine wengi kujeruhiwa kwa mujibu wa maafisa nchini humo. Waziri wa kawi, Taner Yildiz, amesema kuwa zaidi ya wafanyikazi 780 walikuwa katika mgodi huo pale kuliposikika mlipuko katika kitengo cha kusambazia umeme. (J M)
Waokoaji wanajaribu kila mbinu kuwafikia mamia ya wachimba migodi. Inahofiwa kuwa wachimbaji mgodi wengine wengi bado wamefukiwa chini ya mgodi huo. Inakadiriwa kuwa wakati mlipuko huo ulipotokea wafanyikazi 780 walikuwa ndani ya mgodi huo japo inaaminika wengi waliweza kukimbilia usalama wao Bado idadi ya walionaswa ndani ya mgodi huo haijabainika.
 Mgodi huo uko katika mji wa Soma, mkoani Manisa , takriban kilomita 250 kusini mwa Istanbul.
Jamaa za wachimbaji migodi hao wamekusanyika katika makundi karibu na mgodi huo ambao unamilikiwa na wawekezaji wa kibinafsi huku wengi wao wakilia hadharani na kububujikwa na machozi. 
Waziri wa nishati Taner Yildiz ameimabia televisheni ya Uturuki kuwa huenda wengi wamekufa kutokana na sumu ya gesi aina ya carbon monoxide. Amesema moto huo umesababishwa na hitilafu ya umeme.
Picha za televisheni zinaonyesha maafisa wa uokoaji wakiokoa wafanyikazi wa mgodi huo, huku nyuso zao zao zikiwa zimejaa vumbi.Baadhi yao wanaweza kutembea na wengine wanabebwa na kupelekwa ndani ya magari ya kubebea wagonjwa yaliyoegezwa karibu na eneo la tukio.
CHANZO, BBC SWAHILI

MVINYO HAUNA MANUFAA KWA AFYA YAKO



Je umekuwa ukibugia mvinyo ili ili ukusaidie kiafya?
Watafiti wanadai kuwa mvinyo mwekundu (Red wine) hauna manufaa kama ilivyodhaniwa kuwa nayo kwa moyo wa binadamu.
Wanasayansi nchini Italia wamekuwa wakichunguza wenyeji 800 kutoka eneo la Chianti maarufu kwa unywaji wa mvinyo mwekundu nchini humo na kubaini kuwa mvinyo huo hauna faida yeyote kama ilivyodhaniwa awali. (J M)
Aidha watafiti hao wamegundua kuwa kirutubisho cha mvinyo huo ''Resveratrol'' hakizuii maradhi ya moyo wala kurefusha maisha ya wale wanayoikunywa mvinyo huo mwekundu.
wafaransa ni waraibu wa vyakula vya kukaangwa kwa mafuta mengi na wanywaji wa mvinyo.
Utafiti wa awali umekuwa ukiashiria kuwa unywaji huo wa mvinyo mwekundu ulaji wa chocolate na matunda labda ndiyo huzuia maradhi ya moyo.
Watafiti waligundua kuwa kiungo cha Resveratrol ndicho kibwagizo katika vyakula hivyo vyote na hivyo kuipigia debe kuwa ndiyo sababu ya afya nzuri ya wafaransa.
Lakini Prof Richard Semba, kutoka chuo kikuu cha Johns Hopkins ameshindwa kuthibitisha hilo.
Aliwaongoza madaktari watafiti wa maradhi ya moyo kuwachunguza wakongwe 783 kutoka mji wa Tuscany ambao walitoa maelezo kuhusu siha zao vyakula wanavyokula na kunywa na hata mkojo ili kufanyiwa utafiti na kwa zaidi ya kipindi cha miaka 9.
Katika kipindi hicho cha miaka 9 wakongwe 268 walioshiriki katika utafiti huo waliaga dunia 174 walipata maradhi ya moyo na wengine 34 walipatikana wameathirika na ugonjwa wa saratani.
Resveratrol haikuonekana kusaidia katika matukio hayo yote na hivyo kutilia shaka faida yake mwilini.
Daktari wa moyo nchini Uingereza Maureen Talbot,anasema licha ya ripoti hiyo wakfu wa magonjwa ya moyo nchini Uingereza hautabadilisha ushauri wake kwa umma kuwa watu waendelee kula mboga matunda na nafaka.

NIGERIA YAKATAA MASHARTI YA BOKO HARAMU


Nigeria imekataa masharti yaliyowekwa na kiongozi wa Boko Haramu, Abubakar Shekau kwa ajili ya kuwaachia huru wanafunzi wa kike zaidi ya 200 waliotekwa na wanamgambo wa kundi hilo.

Zaidi soma => http://bit.ly/BokoHaram2 (J M)

WAZIRI AKWEPA HOJA ,AMSHAMBULIA LISSU

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan alikataa kueleza walipo waasisi sita wa Muungano ambao kambi ya upinzani ilidai kuwa waliuawa na kuzikwa handaki moja, badala yake akatumia nafasi hiyo kumshambulia mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu akidai hizo ni propaganda na upotoshaji.
Juzi wakati akiwasilisha hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani, Lissu aliitaka Serikali kutoa maelezo bungeni kuhusu sababu za kuuawa kwa waasisi sita wa Muungano wa Tangayika na Zanzibar na kuzikwa katika handaki moja visiwani Zanzibar.
Lissu aliwataja waasisi hao kuwa ni Abdalah Kassim Hanga, aliyekuwa waziri mkuu, Abdul Aziz Twalam aliyekuwa Waziri wa Fedha na Abdulaziz na Saleh Akida aliyekuwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar.(P.T)
Pia aliwataja Othman Shariff, Mdungi Ussi na Jaha Ubwa ambao alisema nao waliuawa na kuzikwa katika handaki moja eneo la Kama nje kidogo ya Zanzibar.
"Tunataka kujua ukweli kama walifanya makosa, walishtakiwa katika mahakama gani iliyowahukumu adhabu ya kifo... tunataka kuambiwa ukweli kwanini mchango wao kuhusu Muungano umefichwa," alisema Lissu juzi.
Lakini alipoulizwa kuhusu madai hayo, Waziri Hassan alionekana kuzigeuza hoja hizo kuwa ni za Lissu pekee badala ya kambi ya upinzani na kumshambulia mbunge huyo akidai kuwa ni mpotoshaji, anayepiga propaganda na mchochezi.
Waziri huyo, ambaye ni Mzanzibari, alisema alipuuza maswali yote kuhusu waasisi hao akisema mbunge huyo wa Chadema alipotoka katika hotuba yake na ndio maana hakutaka kuzungumzia katika majumuisho ya bajeti ya ofisi yake bungeni.
"Yule Lissu sio mkweli na ndio maana sisi tulimpuuza," alisema waziri huyo.
"Hakuna kitu kama hicho na endapo kingekuwepo sisi Serikali tungeshatoa ufafanuzi ili watu wapate kujua ukweli wake," aliongeza Waziri Samia bila kutoa ufafanuzi wa nini kiliwatokea watu hao walioshika nafasi za juu serikalini mara baada ya Mapinduzi na Muungano wa Zanzibar na Tanganyika.
Pamoja na kudai kuwa aliona hoja hizo ni upotoshaji, Waziri huyo, ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa Bunge la Katiba, aliwasihi wabunge wa upinzani kupeleka hoja zao katika Bunge Maalumu la Katiba linalojadili uundwaji wa Katiba Mpya, ambalo pia limetawaliwa na suala la muundo wa Muungano na kero zake.
Waziri Samia alisema hoja hizo zinalenga kuwaaminisha Watanzania mambo ambayo hayapo ili kuwajaza chuki dhidi ya Serikali yao na pia alidai zina uchochezi ndani yake.
Waziri Samia aliwashauri wabunge pamoja na Watanzania kupuuza kauli hizo akidai mbunge huyo hautakii mema Muungano na ndio maana anaibua mambo aliyodai kuwa ni ya uongo na ya uchochezi.

USIOMBEE KUUGUA DENGUE KIPIMO SH.50,000 

Waombolezaji wakibeba jeneza lenye mwili wa Daktari Gilbert Buberwa wa Hospitali ya Temeke kwa ajili ya kuagwa. Daktari huyo, aliyefariki kwa kuugua homa ya dengue, anatarajiwa kuzikwa leo jijini Dar es Salaam. Picha na Rafael Lubava
Wakati taharuki iliyosababishwa na mlipuko wa homa ya dengue ikiendelea kutikisa kila kona ya jiji, imebainika kwamba gharama za vipimo katika hospitali mbalimbali zinafikia Sh50,000, ikiwa ni tofauti kubwa na Sh1,000 kwa kipimo cha malaria.
Ugonjwa huo unazidi kusambaa jijini Dar es salaam na baadhi ya mikoa, kiasi cha mamlaka kuagiza mabasi yote yaendayo mikoani yafanyiwe usafi wa kunyunyizia dawa za kuua wadudu kudhibiti usienee zaidi mikoani. Pia wananchi wameshauriwa kuvaa nguo ndefu ili kudhibiti mbu wanaoeneza ugonjwa huo mchana tofauti na mbu wa malaria.
Timu ya waandishi wa Mwananchi ilipita katika baadhi ya hospitali kubwa binafsi na za Serikali jijini Dar es Salaam na kubaini kuwa gharama ya kupima homa hiyo ni kubwa zaidi katika hospitali na vituo binafsi vya afya, lakini wagonjwa wanaokwenda katika hospitali za Serikali hulazimika kulipa kati ya Sh25,000 na Sh30,000. Pamoja na homa hiyo kufananishwa na malaria kwa dalili na kuenezwa na mbu, gharama za vipimo vyake ni tofauti kwani mgonjwa wa malaria hutozwa kati ya Sh1,000 na 2,000.
Hata hivyo, jambo la kutia moyo ni kwamba baada ya mgonjwa kupata majibu na kubainika anaumwa homa ya dengue, gharama za tiba huwa ndogo kati ya Sh200 na 500 za kununulia dozi ya dawa za kutuliza maumivu aina ya panadol.
Wanaopima waongezeka(P.T)
Mchunguzi wa magonjwa katika maabara ya kimataifa ya Lancet, Kanda ya Tanzania, Mohamed Abdulai alisema idadi kubwa ya watu wanakwenda katika maabara hiyo kupima homa ya dengue tangu ugojwa huo uenee kwa kasi kati ya Machi na Aprili mwaka huu.
Alisema kwa siku wagonjwa zaidi ya 40 hupima dengue na katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja, wagonjwa 53 waligundulika kuwa na homa hiyo.
Abdulai alisema gharama za kipimo cha dengue katika kituo hicho ni Sh50,000.
Katika Hospitali ya Aga Khan, Mkurugenzi wa Tiba, Dk Jaffer Dharsee alisema kipimo cha homa ya dengue ni kati ya Sh35,000 hadi Sh40,000 kutokana na mchakato wa upimaji wake.
"Ni lazima tunapompima mtu dengue pia tumpime na maradhi mengine kwanza kama homa ya matumbo, malaria na maradhi mengine ambayo tunahisi anayo na ndiyo gharama inakuwa kubwa," alisema Dk Dharsee.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Hindu Mandal, Dk Kaushik Ramaiya alisema katika hospitali hiyo kipimo cha homa ya dengue ni Sh30,000. "Tunatumia vipimo vitatu, kile kitakachoangalia iwapo chembe hai nyeupe za damu zimepungua, malaria na kiwango cha sumu kinachotokana na virusi vya dengue," alisema.
Dk Ramaiya alisema tangu vyombo vya habari vianze kuripoti ugonjwa huu, watu wamejawa hofu na hufika hospitali kwa wingi wakitaka kupima maradhi hayo ili kujua kama wapo salama