TIFFAN ENT

TIFFAN ENT

TUKO WANGAPI

TUKO WANGAPI

GLORY FREIGHT

GLORY FREIGHT

Friday, September 12, 2014

JK ATAKA MSAADA ESRF KUONDOA UMASKINI KWENYE UCHUMI UNAOKUA 

DSC_0039
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi Huru ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF), Dk. Hoseana Lunogelo akisalimiana na Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini , Alvaro Rodriguez nje ya ukumbi wa mikutano kabla ya mgeni rasmi kuwasili kwenye mkutano mkubwa wa tatu wa ESRF unaozungumzia ukuaji wa uchumi kwa kutumia fursa zilizopo na maendeleo yanayogusa jamii uliofanyika jana jijini Dar katika hoteli ya Hyatt Regency, Kilimanjaro.(Picha zote na Zainul Mzige wa MOblog)
Na Mwandishi wetu
RAIS Jakaya Kikwete amewataka nguli wa masuala ya uchumi na maendeleo ya binadamu kuisaidia serikali kufanikisha azma yake ya maendeleo kwa wananchi hasa ikizingatiwa kwamba zipo raslimali za kutosha, uchumi unakua lakini umaskini haupungui.
Rais alisema hayo jana wakati akifungua mkutano mkubwa wa tatu wa Taasisi Huru ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) unaozungumzia ukuaji wa uchumi kwa kutumia fursa zilizopo na maendeleo yanayogusa jamii uliofanyika hoteli ya Hyatt Regency, Kilimanjaro.
Katika hotuba yake kwa wataalamu nguli hao ambao wanaangalia athari za kisera na kutoa ushauri katika masuala ya maendeleo yenye kulenga kunufaisha jamii, alisema katika miaka 10 iliyopita uchumi wetu umekua ukikua kwa kasi lakini hali hiyo haikuweza kusaidia kupunguza umaskini kama ulivyolengwa na serikali...(MC)
Alisema moja ya malengo ya millennia yalikuwa ifikapo mwaka wa kesho hali ya umaskini ipunguzwe angalua nusu yake, kwa kuongeza pato la mtu binafsi lakini hali sivyo ilivyo.
Rais ambaye alitumia muda mwingi kueleza maendeleo ya kiuchumi yaliyofikiwa katika hatua ya kuifikisha nchi hii miongoni mwa mataifa yenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025, alisema zinatakiwa juhudi kubwa ili kuondoa umaskini wa kipato kwa mtu mmoja mmoja.
DSC_0047
Mwenyekiti wa Bodi ya ESRF, Philemon Luhanjo (kushoto) akiteta jambo na Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez nje ya ukumbi wa mikutano kwenye hoteli ya Hyatt Regency, Kilimanjaro.
“Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika ustawi wa jamii kama uandikishaji wa watoto shule, uzazi na upunguzaji wa vifo vya watoto, taifa bado linakabiliwa na changamoto kubwa ya ubora wa elimu, upunguzaji wa vifo kwa wanawake wazazi na utapiamlo” alisema Rais Kikwete.
Alisema kwa kuangalia takwimu hizo katika jamii na ukuaji wa uchumi ni dhahiri kwamba taifa letu ili kufikia malengo yake kuna mambo mengi yanatakiwa kufanyiwa kazi na kuamini kwamba wataalamu hao katika mada zao mbalimbali watakazojadiliana watatoka na kitu cha maana kuisaidia serikali kupata mwelekeo sahihi wa kufikia taifa lenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Dira ya maendeleo ya mwaka 2025 ambayo inayotaka kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati yenye maisha bora, utawala bora na uchumi wenye ushindani miongoni mwa mambo machache yenye upeo wa juu yaliyomo katika dira hiyo ndiyo yanayotumika kujadili na hatimaye kuipa serikali majawabu ya mambo muhimu yanayotikisa safari ya kuelekea huko.
Ili kufika huko kwa mujibu wa Rais Kikwete viashiria kadhaa vitaonekana ikiwa ni pamoja na kushuka kwa mchango wa kilimo kwa pato la taifa na ajira, kukua kwa sekta ya kisasa ya viwanda na huduma kwa uchumi, kukua kwa miji na mabadiliko katika vizazi na vifo ambapo taifa linaondoka katika vifo na uzazi wa fujo na kuwa na vizazi vidogo na vifo kidogo kutokana na kukua kwa elimu na huduma za afya.
DSC_0064
Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF Dk. Hoseana Lunogelo (kushoto) akiongozana na Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini , Alvaro Rodriguez kuelekea kwenye ukumbi wa mkutano.
Alisema mpango wa muda mrefu umelenga ifikapo mwaka 2025 mchango wa kilimo kwa pato la taifa utapungua kutoka asilimia 27.8 kufikia 20.7, mchango wa viwanda kupanda kutoka 24.4 hadi 30.7 na mchango wa huduma utapanda kutoka asilimia 47.8 ya mwaka 2010 hadi 48.6.
“Ni matumaini yangu kwamba wastani wa idadi ya watu ikipungua kutokana na elimu na huduma safi za afya au ukuaji wa kasi wa pato la taifa kuliko ongezeko la watu na hivyo kipato kitaongezeka na umaskini utapungua”
Miaka 10 iliyopita mchango wa kilimo katika pato la taifa umekuwa mkubwa huku vizazi na vifo vikiwa ni vingi.
Mkutano huo ambao unajadili mabadiliko ya kiuchumi kwa ajili ya maendeleo ya jamii unatokana na ripoti ya mradi wa maendeleo ya jamii (THDR) iliyofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
DSC_0025
Wageni waalikwa wakipitia ripoti mbalimbali zilizoandaliwa na ESRF nje ya ukumbi wa mikutano kabla ya kuwasili kwa mgeni rasmi.
Naye Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini , Alvaro Rodriguez akizungumza kwa niaba ya Umoja wa Mataifa katika mkutano huo amesema Umoja wa Mataifa utaendelea kuisaidia Tanzania kutengeneza ustawi kwa wananchi wake.
Alisema pamoja na kuwapongeza ESRF kwa kuandaa mkutano huo muhimu wa kuipatia serikali fikira za namna ya kuboresha hali za wananchi wake.
Alisema amefurahishwa kwa ESRF kusaidia kutafuta mustakabali wa maendeleo kwa minajili ya kuendeleza wananchi kwani maendeleo ya kweli ni yale yanayoboresha maisha ya wananchi.
Aidha alivitaja vigezo muhimu vya maendeleo ya jamii katika hali ya uchumi unaokua ambavyo ni kuhakikisha kwamba kuna usawa katika ukuaji wa uchumi na maisha ya wananchi, kuongeza uwezo wa kuhami maendeleo yaliyofikiwa dhidi ya haki zisizotabirika zinazovuruga ustawi,Kuhakikisha maendeleo endelevu ya wananchi na nchi na kuendelea kuwasaidia wanaume kwa wanawake kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo iwe kiuchumi, kijamii na kisiasa na kugawana kwa usawa matunda ya maendeleo.
DSC_0068
Mratibu wa Programu kutoka ESRF, Yasser Manu (kulia) akibadilishana mawazo na baadhi ya wafanyakazi wenzake nje ya ukumbi wa mikutano kabla ya kuwasili kwa mgeni rasmi.
Amesema Mratibu huyo wa mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini kwamba amefurahishwa na taarifa kwamba mkutano huo utajadili mada mbalimbali na kutolea ushauri kwa kuzingatia taarifa ya THDR.
Awali akimkaribisha Mwenyekiti wa Bodi ya ESRF Philemon Luhanjo, kumkaribisha rais Jakaya Kikwete Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF Dk Hoseana Lunogelo alisema wakati taasisi hiyo inaadhimisha miaka 20 ya uwepo wake, katika mkutano wake wa 3 wa kitaifa wanatarajia wanazuoni kuchambua mada mbalimbali na kuandika kitu kitakachosaidia serikali katika kuhakikisha maendeleo ya kiuchumi yanakwenda sanjari na ustawi wa jamii kwa maana ya kuondokana na umaskini katika ngazi ya mtu mmoja mmoja.
Mada zinazochambuliwa zinatoka kwa wataalamu waliobobea kutoka Tanzania,Ethiopia, Uingereza, Norway na India.
DSC_0195
Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dk. Hoseana Lunogelo akibadilishana mawazo na Balozi wa Japan nchini Tanzania,Mh. Masaki Okada wakati wakimsubiri mgeni rasmi kuwasili ukumbini hapo.
DSC_0203
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akilakiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya ESRF, Philemon Luhanjo mara baada ya kuwasili kwenye hoteli ya Hyatt Regency, Kilimanjaro kufungua mkutano mkubwa wa tatu wa Taasisi Huru ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) unaozungumzia ukuaji wa uchumi kwa kutumia fursa zilizopo na maendeleo yanayogusa jamii.
DSC_0204
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez.
DSC_0209
Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dk. Hoseana Lunogelo (kushoto) akiongozana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (kulia) pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya ESRF, Philemon Luhanjo (katikati) kuelekea ukumbi wa mikutano.
DSC_0233
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwasili ukumbini kufungua mkutano mkubwa wa tatu wa Taasisi Huru ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) unaozungumzia ukuaji wa uchumi kwa kutumia fursa zilizopo na maendeleo yanayogusa jamii. Katikati ni Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez.
DSC_0251
Meza kuu, Katikati ni mgeni rasmi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya fedha, Prof. Adolf Mkenda, Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez ( wapili kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya ESRF, Philemon Luhanjo (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dk. Hoseana Lunogelo (wa pili kushoto).
DSC_0280
Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dk. Hoseana Lunogelo akisoma taarifa ya taasisi yake mbele ya mgeni rasmi wakati wa mkutano mkubwa wa tatu wa ESRF unaozungumzia ukuaji wa uchumi kwa kutumia fursa zilizopo na maendeleo yanayogusa jamii sambamba na kutimiza miaka 20 ya tasisi hiyo tangu kuanzishwa kwake uliofanyika jana jijini Dar katika hoteli ya Hyatt Regency, Kilimanjaro.
DSC_0295
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akitoa mkono wa pongezi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dk. Hoseana Lunogelo mara baada ya kusikiliza taarifa ya maendeleo ya ESRF.
DSC_0301
Mwenyekiti wa Bodi ya ESRF Philemon Luhanjo, akizungumza neno fupi kabla ya kumrabisha mgeni rasmi Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufungua rasmi mkutano huo.
DSC_0389
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akifungua rasmi mkutano mkubwa wa tatu wa ESRF unaozungumzia ukuaji wa uchumi kwa kutumia fursa zilizopo na maendeleo yanayogusa jamii uliofanyika jana jijini Dar katika hoteli ya Hyatt Regency, Kilimanjaro.
DSC_0349
DSC_0455
Mkurugenzi wa Programu wa ESRF ambaye pia ni Mratibu wa Mradi wa taarifa ya maendeleo ya watu nchini Tanzania (THDR), Dr. Tausi Kida akifuatilia kwa makini hotuba ya mgeni rasmi (hayupo pichani) wakati wa mkutano huo.
DSC_0393
Mjumbe wa Bodi ya wadhamini ESRF, Prof. Sylvia Temu akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi.
DSC_0444
Mratibu Mkazi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini, Alvaro Rodriguez akizungumza kwa niaba ya Umoja wa Mataifa wakati wa mkutano huo. Kulia ni Gelase Mutahaba kutoka Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Kushoto ni Prof. Bertil Tungodden kutoka nchini Norway na Mjumbe wa Bodi ya wadhamini ESRF, Prof. Sylvia Temu (wa pili kushoto).
DSC_0257
Pichani juu na chini ni Baadhi ya wawakilishi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa nchini, mabalozi, taasisi mbalimbali za serikali waliohudhuria mkutano huo uliofanyika kwenye hoteli ya Hyatt Regency, Kilimanjaro jijini Dar.
DSC_0265
DSC_0259
DSC_0267
Kwa picha zaidi MOblog.....(MC)

Vikwazo dhidi ya Urusi kuanza rasmi leo


Vikwazo vya Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi vitaanza rasmi kutumika leo.
Hata hivyo, vitaondolewa vyote au baadhi yake tu mwezi ujao iwapo kutakuwa na maendeleo katika utekelezaji wa mpango wa amani wa Mashariki mwa Ukraine.
Uamuzi wa kutekeleza vikwazo hivi ulifikiwa jana baada ya mkutano wa pamoja kati ya waziri mkuu wa Uingereza David Cameron na viongozi wengine mashuhuri wa EU.
Mchakato huu ulicheleweshwa kwa siku kadhaa kwa hofu ya baadhi ya nchi kwamba vikwazo zaidi vitaharibu matarajio ya kusitishwa mapigano.
Vikwazo hivi vipya vinayalenga makampuni ya mafuta ya Urusi, sekta za fedha na ulinzi.
Pia wameongeza majina mengine 24 katika orodha ya maafisa wa Urusi na viongozi wa waasi nchini Ukraine ambao wanakabiliwa na kunyimwa visa na kuzuia mali zao.
CHANZO; BBC SWAHILI

 

Mfungwa apatikana na simu mwilini Kenya


Kwa baadhi ya watu simu ya mkononi ni kifaa tu cha mawasIliano ilihali kwa wengine ni kifa ambacho kinaweza kukuweka katika hali ya kufa kupona.
Mfungwa mmoja nchini Kenya amewaacha wengi vinywa wazi, baada ya simu tatu za mkononi kutolewa mwilini mwake. Inaarifia aliziingiza simu hizo mwilini mwake kupitia sehemu yake nyeti ya nyuma.
Mfungwa huyo wa gereza la King'ong'o katika jimbo la Nyeri alifanyiwa upasuaji Jumanne kutolewa simu hizo ambazo alikuwa amezificha mwilini mwake kupitia sehemu yake ya nyuma.
Mfungwa ambaye alitolewa simu mwilini kwa kufanyiwa upasuajiTatizo la kuingiza bidhaa kimagendo ndani ya magereza ni kero kubwa kwa maafisa wakuu wa magereza.
Wamekuwa kwa miaka mingi wakijaribu kulikomesha tatizo hilo bila mafanikio.Kwa njia yoyote ile wafungwa huingiza bidhaa kama simu katika magereza nchini Kenya kinyume na sheria za magereza.
Maafisa wa magereza wanakiri kwamba wafungwa hawa wakati mwingine hushirikiana na walinzi wa magereza kuingiza bidhaa katika magereza kimagendo.
CHANZO; BBC SWAHILI

 

Wednesday, September 10, 2014

TAMISEMI YATAKA KUONGEZA ZAIDI KIWANGO CHA TAHADHARI YA UGONJWA WA EBOLA.

 Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Godfrey Mtei akipokea zawadi ya saa ya ukutani kutoka kwa Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia, juzi mjini hapa.
 picha ya pamoja .
 Picha ya pamoja baadhi ya waganga wakuu wa wilaya na mikoa wakiwa na Mgeni rasmi , Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia.
 Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia akikambishi zawadi ya saa ya ukutani Mganga Mkuu wa Serikali,Dk Donan Mmbando,saa hiyo iliyolewa na Taasisi ya Lab Eguip Limited.
 Baadhi ya waganga wakuu wa wilaya na Mikoa ya Tanzania Bara wakisiliza hotuba ya Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia ( hayupo pichani).
 Dk Frida Mokiti ( kushoto) akibadilishana mawazo na mwezake wakati wa mapumziko
Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia, akiwa na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Donan Mmbando , baada ya waziri kufungua mkutano.

Na John Nditi, Morogoro
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),Hawa Ghasia, amewaagiza  Waganga Wakuu wa Mikoa , na Halmashauri za wilaya nchini kuongeza zaidi kiwango cha kuchukua tahadhari katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ukiwemo wa Ebola.
Waziri Ghasia alitoa agizo hilo jana mjini hapa wakati wa  hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa mwaka wa Waganga wakuu wa mikoa, Halmashauri za wilaya na wakurugenzi wa Hospitali za rufaa kutoka mikoa yote ya Tanzania bara.
Kwa mujibu wa Waziri huyo kuwa, hapa nchini ugonjwa huo  haujathibitika kuingia na Serikali imechukua tahadhari zote kuhakikisha kuwa ugonjwa huo hauingii  nchini na endapo utathibikika kuingia uweze kudhibitiwa kikamilifu.
Hata hivyo alisema , mwaka huu kumekuwepo na matukio ya hapa nchini na nje ya nchi yaliyotufanya tuongeze zaidi kiwango cha tahadhari , na tukio la kwanza ni la mlipuko wa ugonjwa wa Dengue , ambao uliwapata wagonjwa 1,384 kote nchini, na kusababisha vifo vya watu wanne , sehemu kubwa ya wagonjwa walikuwa ni wa Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Waziri huyo , tukio la pili ni la ugonjwa wa ebola ,ambao kwanza ulianzia nchi za Afrika Magharibi,  na kati ya Machi hadi Agosti mwaka huu , watu 3,069 waliungua ugonjwa huo.
Hivyo  hadi kufikia Agosti 28, mwaka huu ,ugonjwa huo umeua watu 1,552 na hivi karibuni umeingia nchi ya Congo DRC na kufikia mwishoni mwa mwezi uliopita watu 24 wameripitiwa kuugua .
“ Ni matumaini yangu kuwa katika mkutano huu  , suala la magonjwa ya mlipuko kama haya yatajadilikwa kikamilifu ili kila mmoja wenu awe katika tahadhari kubwa” alisisitiza Waziri Ghasia
Hata hivyo , Waziri Ghasia alitumia fursa hiyo kutoa shukrani za Serikali ya Tanzania kwa Watu wa Marekani kupitia Shirika lao la CDC na Shirika la Afya Duniani kwa kutoa vifaa na vifaa tiba kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo wa ebola.
Mbali na tahadhari ya magonjwa ya mlipuko, Waziri Ghasia alisema , katika ziara zake sehemu mbalimbali hapa nchini ameshuhudia juhudi zinazofanywa na wadau katika kuboresha upatikanaji  na utoaji wa huduma za afya na ustawi wa jamii.
Kwa mujibu wa Waziri huyo kuwa juhudi hizo ni  kujenga vituo vipya vya huduma za afya , kukarabatiwa vituo ambavyo havipo katika hali nzuri  kuongeza watumishi na upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na kuimalisha utaratibu wa kukusanya mapato katika vituo.
Pia ulimalishaji wa utoaji wa huduma kwa makundi maalumu hususan , wanawake wajawazito, watoto chini ya miaka mitano na  wazee  katika baadhi ya maeneo husika.
Hata hivyo alisema ,kutokana na juhudi hizo, malalamiko kuhusu uhaba wa dawa na vitendo vya rushwa yamepungua katika maeneo ambako juhudi hizo zimekwishafanyika.
“ Nimefurahishwa  na kasi ya ujenzi mpya wa Zahanati na Vituo vya Afya .... juhudi hizi zinapaswa kupongezwa  kwa vile ni utekeleaji wa Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM)” alisema Waziri Ghasia .
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali , Dk Donan Mmbando, kabla ya kumkaribisha waziri , alisema lengo la mkutano huo ni kujadili masuala muhimu yanayolenga kuboresha huduma za afya na ustawi wa jamii hapa nchini na pia kuainisha changamoto mbalimbali zinazowakabili watumishi wa wizara hiyo.
Hata hivyo alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wataalamu hao wa sekta ya afya kujipanga kukabiliana magonjwa ya mlipuko ukiwemo wa ebola na kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya kutolea huduma endapo kutakuwa na udhibitisho wa dalili za wagonjwa katika maeneo yao.
Pamoja na kuzungumzia changamoto zilizopo ikiwemo ya ya  usimamizi wa utendaji bora na uboreshaji wa  mazingira ya kazi na y a watumishi , pia aliwataka wataalamu wao kuangalia namna ya kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukizwa ukiwemo wa saratani.
Kwa mujibu wa Manga Mkuu wa Serikali, kuwa vituo vingi vya Afya vilijengwa kwa kuangalia upande mmoja wa kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza na kusahau mengine yasiyoambukizwa na kwamba hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa ili kukabiliana nayo na kutaka yaingizwe kwenye mpango kazi wa mwaka 2016

KIVUKO CHA MV. KIGAMBONI KUANZA KAZI KESHO KUTWA

Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Watendaji mbalimbali hawapo pichani kutoka, Wizara ya Ujenzi, TEMESA na Kikosi cha Maji cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambao wamefanya kazi kubwa ya ukarabati wa Kivuko cha MV Kigamboni.
Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipanda ngazi kwenda kukagua Kivuko cha MV Kigamboni ambacho matengenezo yake makubwa yanakamilika leo.
Luteni Kanali Gwanafi kulia akimuongoza Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwenda kukagua Kivuko cha MV Kigamboni sehemu ya chini mara baada ya kukamilika kwa ukarabati wake.
Luteni Kanali Gwanafi wapili kutoka kulia akitoa maelezo kuhusu ukarabati mkubwa wa Kivuko cha MV Kigamboni kama inavyoonekana.
Taswira-Kivuko cha MV Kigamboni kinavyoonekana mara baada ya Ukarabati wake.
Luteni Kanali Gwanafi kulia akimuonesha Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli sehemu ya juu ya Kivuko cha MV Kigamboni.
Luteni Kanali Gwanafi kushoto akimuonyesha Waziri wa Ujenzi Dkt. John Magufuli pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Mhandisi Mussa Iyombe kuhusu sehemu ya chini ilivyokarabatiwa.
Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa ndani ya kivuko cha MV Kigamboni huku akipatiwa maelezo kuhusu ukarabati wake.
Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akimsikiliza kwa makini Luteni Kanali Gwanafi kuhusu mambo mbalimbali wanayofanya ndani ya kivuko cha MV Kigamboni.
Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akitoka ndani ya Kivuko cha MV Kigamboni mara baada ya ukaguzi wake. Picha zote kwa Hisani ya Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Ujenzi.


Waziri wa Ujenzi Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa Kivuko cha MV Kigamboni kinatarajiwa kuanza safari zake za usafirishaji rasmi kesho kutwa mara baada ya ukarabati wake kukamilika.

Waziri wa Magufuli alitoa kauli hio leo wakati akikagua kivuko hicho ambacho kilikuwa kikikarabatiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kupitia kikosi cha Wanamaji.

Mheshimiwa Magufuli aliongeza kuwa hicho ambacho kinategemewa na wananchi wengi waishio Kigamboni na maeneo jirani kinategemewa kuteremshwa majini kesho jioni mara baada ya maji kujaa na kesho kutwa kuanza rasmi shughuli zake za usafirishaji.

“Nimekagua na kujionea kazi inavyoendelea na nimeridhishwa na mlipofikia mpaka sasa, naamini kazi imefanyika ipasavyo, hivyo basi palipobaki ni matengenezo madogo, kutokana na utendaji wenu wa kazi naamini kesho Kivuko hicho kitateremshwa majini na kesho kutwa kuanza safari”, Alisema Waziri Magufuli.

Aidha, Mheshimiwa Magufuli alikipongeza kikosi hicho cha Navy kwa kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa wanamaliza ukarabati huo kwa wakati licha ya changamoto nyingi walizokumbana nazo.

Sambamba na hilo, Waziri Magufuli amesema kuwa ndani ya Wiki tatu au nne Boti ya Kutoka Dar hadi Bagamoyo itawasili kwani imeshateremshwa majini huko inapotengenezwa na kilichobaki ni kuifikisha Dar es Salaam

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Mhandisi Mussa Iyombe, amepongeza Jeshi la Wananchi Tanzania kupitia Kikosi cha majini kwa uzalendo wao waliouonesha kwa kukamilisha ujenzi huo kwa gharama nafuu na kwa wakati ili kurejesha huduma za usafirishaji.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Mhandisi Marceline Magessa amesema kuwa ukarabati wa MV Kigamboni ulikuwa katika hatua za marekebisho mbalimbali ikiwemo utoaji kutu, kupaka rangi, usafi na uzibaji wa matundu pembezoni mwa kivuko hicho.

Naye kamanda wa kikosi cha majini Brigedia Jenerali Rogastian Laswai amezitaja changamoto zilizowakabili wakati wa utengenezaji wa kivuko hicho kuwa ni pamoja na kushindwa kupaka rangi kutokana na uwepo wa mvua pamoja na kupwa na kujaa kwa maji

Ukarabati wa Kivuko cha MV Agosti 14 mwaka huu mpaka kukamilika kwake hivi leo.

Monday, September 8, 2014

DR.KHAMIS KINGWANGALLAH ATANGAZA NIA YA KUGOMBEA URAIS 2015

1
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya serikali za Mitaa na Mbunge wa jimbo la Nzega Dr. Khamis Kigwangallah akitangaza nia yake ya kugombea urais waJamhuri ya Muungano ya Tanzania wakati alipokutana na waandishi wa habari kwenye ambapo amesema hajasukumwa na mtu yeyote ila ni yeye mwenyewe ameamua kwa moyo wake.
02
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya serikali za Mitaa na Mbunge wa jimbo la Nzega Dr. Khamis Kigwangallah akimtambulisha mke wake Dr Bayoum Awadh wakati wa mkutano huo.
2
Mzee Nasser SAid Mussa baba mzazi wa Dr. Khamis Kigwangallah na mama yake mzazi Mama Bagaile Lumola.(P.T)
4
Mzee Nasser SAid Mussa baba mzazi wa Dr. Khamis Kigwangallah na mama yake mzazi Mama Bagaile Lumola. na watoto wake Sheila kulia ni Hawa.
8
Mchungaji Patrick Saso akifanya maombi kabla ya kuanza kwa mkutano huo.
9
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo.
10
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo.
DSC_0103
Sheikh Abubakary Mwita akiomba dua kabla ya kuanza kwa mkutano huo.
Ndugu viongozi mlioko hapa, wageni waalikwa, wanahabari na watanzania wenzangu mnaonisikiliza;
Ni heshima kubwa sana kwangu kupata fursa hii. Ni katika nchi chache sana duniani, mtoto wa maskini kama mimi, aliyewahi kutembea mitaani akiuza karanga, Big G, maandazi, jerebi na samaki ili kusaidia wazazi kupata chochote kwa ajili ya kulisha familia anaweza kuota kuwa Rais wa nchi yake. Kwamba, mtoto aliyeenda shule bila viatu anaweza kuwa Daktari.
Hii inamaanisha misingi ya haki na usawa kwa wote iliyowekwa na waasisi wa Taifa hili haikuwa ndoto za alinacha, bali ukweli na uhalisia, na inafanya kazi. Kwamba, siyo lazima uwe mtoto wa tajiri ndiyo uoneshe kipaji chako.
Hili peke yake linanipa sababu ya ziada ya kwa nini nitamani kuota kuwa Rais – nataka niwe mfano hai wa mafanikio ya Ndoto ya waasisi wa Taifa letu, kuwa sote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tuna haki na fursa sawa bila kujali nani anatokea familia ipi. Hii ni Tanzania ya ndoto za waliotutangulia. Ni lazima atokee kiongozi wa kizazi hiki anayetamani kuiongoza Tanzania itakayodumu kwenye misingi hii:
kwamba sisi sote ni ndugu, na tuna fursa sawa. Kwamba, kuendelea kimaisha na kibinafsi ni haki ya binadamu na si hisani. Kwamba, mtoto wa mama ntilie kama nilivyokuwa mimi hapa, ana haki na fursa ya kuwa mbunge ama Rais wa nchi, sawa kabisa na mtoto wa Mbunge.
Kwa namna ya kipekee nichukue fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza waasisi wa Taifa letu kwa kusimamia tunu hizi. Niwashukuru pia viongozi wote walionitangulia kwa kuzilinda, na niahidi nitakuwa wa mwisho kuisaliti nchi yangu kwenye mambo haya.
Leo nimefika hapa kwa sababu chama change kina mfumo mzuri ulioasisiwa na Mwl. Nyerere na umelindwa na Wenyeviti waliomfuatia mpaka na sisi tumeukuta.
Leo nimefika hapa kwa sababu Rais Jakaya Kikwete na wajumbe wenzake wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu walitumia misingi imara iliyowekwa na waasisi wa Chama changu kuamua kuwa nami nina haki ya kuwa Mbunge. Leo nazungumza hapa nikiamini kuwa ni misingi hiyo hiyo itatoa uongozi wa Taifa letu katika awamu ijayo.
Babu yangu Kizaa Baba aliishi Kijijini Goweko, Mlimani, na alikuwa mfugaji mkubwa wa ng’ombe na mrina asali mashuhuri. Yeye na mkewe waliishi maisha ya heshima sana pale kijijini. Hawakuwahi kusoma wala kuajiriwa japokuwa Babu yangu aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya Chama Cha TANU na baadaye CCM katika ngazi ya Kata.
Babu yangu na Bibi yangu kizaa mama waliishi Nzega, na ndiyo walionilea baada ya ndoa ya mama yangu na baba yangu kuvunjika. Walinifundisha mambo mengi, kubwa likiwa ni kujiamini, pia kufanya mambo yangu kwa bidii, uadilifu, umakini na kwa nidhamu ya hali ya juu. Bibi yangu huyu hakusoma shule ya kizungu japokuwa alijifunza kusoma na kuandika. Babu yangu alikuwa mjukuu wa Chifu na hivyo alipata fursa ya kusoma Tabora School miaka miwili mbele ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Alifanya kazi mbalimbali chini ya serikali ya wakoloni, na alishiriki harakati za kuanzishwa na kusambaa kwa chama cha TAA na baadaye TANU. Babu yangu aliamini kuwa “binadamu wote ni sawa na kwamba kila mtu anastahili kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake”, na kwamba ukoloni haukuwa kitu cha sawa, na hivyo kujitawala wenyewe dhidi ya wazungu ilikuwa ni haki yetu; pia aliamini katika elimu, na hivyo alifanya juhudi kusomesha mabinti zake watatu, mama yangu aliishia kwenye ualimu kabla ya kuingia kwenye ndoa. Babu aliamini kuwa Tanzania ya mabinti zake itahitaji wasomi, ndoto ambayo ninaishi kuitekeleza kwa ajili ya mabinti zangu wawili na Kaka yao, HK Jr.
Japokuwa bibi na babu yangu wameishatangulia mbele ya haki, naamini wananitazama na kutabasamu huko waliko.
Ninaishi nikiamini kuwa hadithi ya maisha yangu ni mfano hai kwa maisha ya watanzania wengi. Na kwamba, nina deni la kulipa kwa vizazi vijavyo kwa kuwa mimi ninafaidi matunda ya mti uliopandwa na vizazi vilivyonitangulia. Naliona jukumu la kuhakikisha vizazi vijavyo vinafaidi urithi wa Tanzania kuwa ni la kwangu na wenzangu wa kizazi hiki.
Kazi yangu imenifikisha sehemu nyingi sana za nchi yetu – vijijini na kwenye majiji, imenikutanisha na watu wa kila aina – matajiri kwa maskini, wazee kwa vijana – hakuna hata mmoja kati ya watu hawa anayetegemea Serikali itamtatulia kero zake zote. Wanajua wanapaswa kufanya kazi kwa bidii ili wasonge mbele – na wana nia ya kufanya hivyo.
Nenda kwa wafanyabiashara wakubwa kule Pugu Road viwandani, kwa watumishi pale hospitali ya Taifa Muhimbili, ama pale sokoni Kariakoo kwa wafanyabiashara, wote watakuambia hawapendi kuona kodi zao zikitafunwa na wachache pale TRA, ama kulipa posho za bure kwa wabunge na mawaziri kule Bungeni, kulipia mashangingi ya viongozi na watendaji, kulipia tiketi za ndege daraja la kwanza kwa ajili ya safari za viongozi na wataalamu wetu kwenda kujifunza kupambana na umaskini wakati wakirudi wanauacha uzoefu uwanja wa ndege, ama kulipia semina, warsha na makongamano ya wataalamu ya kuandika sera za MKUKUTA, MKURABITA na kuandaa bajeti zisizotekelezwa kila mwaka.
Watanzania wanataka kupata huduma bora za afya, elimu, maji, miundombinu.
Nenda kule kwa watani zangu, Nanyumbu, ama Tandahimba, ama kwa ndugu zangu kule Nduli, Kyela, wazee kule watakuambia hawategemei Serikali itawaletea ubwabwa kwenye sahani za fedha, wanajua Serikali haitowafanyia kila kitu, lakini wanajua kabisa kuwa wanapaswa kufanya kazi kwa bidii na wamekuwa wakifanya hivyo siku zote.
Wanachohitaji wao ni kujengewa mazingira wezeshi kushiriki shughuli zao za kilimo ama biashara, waelekezwe namna ya kuongeza uzalishaji kwa kutumia njia za kisasa za kilimo chenye tija na ufanisi, waelekezwe wanapataje pembejeo, wanapataje mikopo yenye riba nafuu, wanahitaji, mwisho wa siku, wajue wapi watauza mazao yao kwa uhakika na bila kudhulumiwa wala kucheleweshewa malipo.
Watu hawatarajii serikali itabeba mizigo yao yote. Lakini wanaamini kabisa, kwamba tukibadili kidogo tu vipaumbele vyetu, tukibadili namna tunavyoendesha serikali, tukibadili kidogo namna tunavyoendesha uchumi wetu, tutaweza, kwa kiasi kikubwa, kubadili muelekeo mzima wa maisha ya baadaye ya watoto na wajukuu zetu. Tutatoa uhakika wa kuiondoa nchi yetu kutoka miongoni mwa nchi maskini kabisa duniani.
Na mimi, kama watanzania wenzangu wengi, nina imani kubwa kabisa, kwamba tunaweza kubadili mustakabali wa Taifa letu. Tunaweza kufungua milango ya maisha bora zaidi kwa watanzania. Tutatoa fursa sawa kwa kila mtanzania kuishi kwa matumaini, kwamba atabadili maisha yake wakati wowote ule kuanzia leo.
Tutaweza kuamsha ari ya kila mtanzania kuongeza bidii kwenye kazi akitumaini na kuamini kuwa kesho yake itakuwa bora kuliko jana yake, kuwa naye ataishi kwa heshima, raha na starehe ndani ya nyumba yake.
Ninaamini, kutokea ndani kabisa ya mifupa yangu, kuwa tukifanya uchaguzi sahihi wa vipaumbele vyetu, tukibadili namna tunavyoendesha serikali yetu, haya ninayoyasema si ndoto za mchana. Ni mambo yanayowezekana.
Watanzania wengi wanaamini, kuwa tukifanya uchaguzi sahihi wa vipaumbele vyetu, mabadiliko makubwa, na ya haraka yatatokea kwenye uchumi wetu. Wanaamini tukichagua kiongozi sahihi mwakani, anayejua mahitaji ya nchi yetu kwa sasa na baadaye, tutafanikiwa.
Nyote mliopo hapa na wanaotusikiliza kutokea nje ya hapa mna jukumu la kututazama kwa ukaribu sana, kututathmini na kutupima sote; tuliojitokeza hadharani, walioanza safari za matumaini, wanaotajwa tajwa, na wale wanaosubiri kuoteshwa ili wakati muafaka ukifika muwape taarifa sahihi watanzania, kuwa kati yetu sote, ni nani anafaa kutuongoza kuelekea Tanzania ya ndoto zetu!
Kuwa, ni nani kati yetu ataweza kuwa Amiri-jeshi-mkuu, siyo kwa uanajeshi wake bali kwa uwezo na utayari wake wa kuwashirikisha wataalamu wa majeshi na kuamua kwa busara kutumia nguvu za kijeshi pale inapolazimika baada ya kupima na kuchambua aina nyingine zote za kutafuta suluhu za migogoro kabla ya kuamua vita.
Kuwa, ni nani kati yetu anayeamini katika uhuru, haki na usawa na wajibu wa watu wote, kama unavyolindwa na Katiba, anayeamini katika haki ya kuabudu lakini asiyekuwa tayari kuitumia haki hiyo kuwagawa watanzania kutokana na dini zao.
Kuwa, ni nani kati yetu anayeamini katika Haki ya kupata huduma bora za afya, elimu, maji, kama wanavyopata wabunge na mawaziri wetu, kama wanavyopata mahakimu na majaji wetu, kama wanavyopata wafanyabiashara na wakurugenzi wetu.
Kuwa, ni nani kati yetu ataweza kuhakikisha kuwa watanzania wote wanapata haki hizi bila kutazama hali zao kiuchumi ama daraja zao kijamii.
Kuwa, ni nani kati yetu anaamini zaidi katika uhuru na kujitegemea kwenye masoko na malighafi ili kudhibiti uchumi wetu mpana wa ndani, kujitegemea kwenye masoko ya pamba na nguo, kwenye mafuta ya kula, kwenye chakula cha uhakika kwa ajili ya watu wetu, kwenye mafuta na gesi ili tukwepe mtego wa kuwa sehemu ya uchumi, masoko na biashara za hasara na faida za makampuni makubwa ya kimataifa nje ya mipaka yetu.
Ili tulinde thamani ya fedha yetu, ili tuwe na uhakika wa ustawi wa maisha ya watu wetu ndani ya nchi bila athari kubwa kutoka nje ya nchi yetu.
Kuwa, ni nani miongoni mwetu anaakisi taswira sahihi zaidi ya watanzania walio wengi, historia yake, rekodi yake, wajihi wake, mtazamo wake, ndoto zake, zinaakisi ‘utanzania’ halisi. Kuwa, yeye ni hitaji sahihi la watanzania.
Wakati ukifika, muwaeleze watanzania ukweli, wafanye uamuzi unaotokana na taarifa sahihi, wachague mtu sahihi.
Mimi, Ndugu zangu, natangaza rasmi sasa, kuwa ninatia nia ya kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2015.
Na nimefikia uamuzi huu bila kuelekezwa, kusukumwa, kushawishiwa, kupangiwa ama kupanga na mtu ama na kikundi cha watu, bali kwa utashi na utayari wangu. Na ninayasema haya, haswa baada ya kutafakari mambo mengi kwa kina:
mahitaji ya sasa na baadaye ya Tanzania ya ndoto zangu, uwepo wa fursa ya kugombea na kushinda uchaguzi ujao, uwezo wangu wa kuchambua mambo, kutafakari, kufanya maamuzi sahihi, kuchukua hatua za utekelezaji na kusimamia utekelezaji, uadilifu na uzalendo wangu, na zaidi nia yangu ya kuwa sehemu ya watanzania wengi tunaotaka kuona mapinduzi ya kifikra katika nchi yetu – mapinduzi ambayo yatatia chachu ya mabadiliko ya namna tunavyochagua vipaumbele vyetu kama Taifa na namna tunavyosimamia utekelezaji wa mambo mazuri tunayojipangia kama Taifa.
Ninatangaza nia ya kugombea Urais nikiwapa fursa watanzania wanipime na kunitazama mwenendo na uwezo wangu, nikiamini kabisa nitapimwa na kuungwa mkono ama kutoungwa mkono si kwa rangi ya ngozi yangu, si kwa jinsi yangu, si kwa umri wangu, na wala si kwa daraja langu kwenye jamii, dini yangu, ama kabila langu. Ninaamini nitapimwa kwa sifa na uwezo wangu, kama mtanzania.
Watanzania tuna sifa moja kubwa; kwenye mambo ya msingi ya kitaifa, tunakubaliana kuwa maslahi ya Tanzania hupanda juu ya maslahi yetu binafsi. Tudumishe utanzania wetu.
Ninaamini katika Ndoto ya Tanzania. Kuwa leo miaka 50 ya kuwa Jamhuri ya Tanzania tuna kila sababu ya kuwa Taifa la dunia ya kwanza, viongozi waliotutangulia wameandaa misingi ya kuifikisha Tanzania kwenye matamanio yetu. Kizazi chetu cha kina jukumu na wajibu wa kuikimbiza Tanzania kufikia kwenye ahadi inayotokana na ndoto za wazee na waasisi wa Taifa letu. Binafsi, niko tayari kulibeba jukumu hilo bila woga wala wasiwasi, maana naamini tusipojitokeza watu kama mimi, tutajikuta tunaongozwa na watu wasiostahili. Nina suluhu ya changamoto kubwa za leo na kesho:
kupigana na njaa na kuhakikisha usalama wa chakula kwa watu wetu, tatizo la ajira kwa vijana na changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi ni miongoni mwa mambo ambayo kizazi chetu kitapaswa kuyafanyia kazi kwa haraka na umakini wa hali ya juu.
Mimi ninaamini kwamba, kama hata mimi nimefika hapa, basi kila mtanzania anaweza, na ana haki ya kufika hapa na kwenda mbele zaidi yangu. Mafanikio siyo haki ya wachache, ni tunu ya Mwenyezimungu kwa kila mtu. Ninaamini ni haki ya kila mtanzania kuota ndoto yake, kuifanyia kazi na kuifikia. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina wajibu wa kutoa fursa kwa watu wake kuota ndoto zao na kufikia mafanikio bila kukwama.
Na ndugu watanzania wenzangu, amini nawaambia, kuwa, mbele yetu tuna kazi ya ziada ya kufanya. Kazi ambayo ninaamini tunaiweza tukiamua; uwezo tunao, sababu tunazo na nia tunayo – sema tuna mapungufu makubwa kwenye kuchukua hatua za kutenda.
Mimi naamini kwamba; E Pluribus unum. Baina ya wengi, mmoja!
Kwamba; Mimi ni mmoja kati ya uwingi wetu. Siwezi kuwa salama kama wengine hawako salama, siwezi kuwa na raha kama wengine wanateseka. Ninaongozwa na ile dhana kwamba, matatizo ya mwenzangu, ni ya kwangu, na si yangu peke yangu, ni yetu sote kama jamii moja.
Hivyo:
- kitisho cha njaa ya familia fulani maskini kule Sakasaka, wilayani Meatu, ni kitisho changu na familia yangu, hata kama siyo familia yangu.
- Kucheleweshewa haki ya kuhukumiwa kwa mtuhumiwa wa mauaji ya kule Sombetini, ni kitisho kwangu pia, hata kama kesi siyo yangu.
- Mzee Makame wa kule Wete, Pemba, aliyefiwa na watoto wake akakosa msaada na yeye hana nguvu za kuzalisha tena, anavyokula mlo mmoja kwa siku ili asukume siku, inaniumiza na kunigusa moyoni, hata kama yeye siyo babu yangu.
- Mama John ni mpishi mzuri wa wali nazi kwa maharage, na ana wateja wengi mtaani kwake maeneo ya Mtaa wa Sikukuu, Sokoni Kariakoo; akifukuzwa, akapigwa virungu, akanyang’anywa pesa zake, akadhalilishwa na kumwagiwa chakula chake na mgambo wa jiji la Dar es salaam kwa kuwa anafanya biashara mahala pasiporuhusiwa, inaniumiza na kunigusa moyoni, hata kama yeye si mama yangu.
- Kama kuna mtoto asiyejua kusoma na kuandika kule Mrijo Chini kwa watani zangu warangi, hiyo inaniuma na kunigusa sana moyoni, hata kama yeye si mwanangu.
- Bwana Kalumanzila ni mmachinga nguo za mitumba mitaani. Yeye huchukua nguo zake kumi kwa kuaminiwa na mwenye belo kutokea soko la Karume, akiuza anachukua kifaida kidogo cha juu kinachozidi hapo juu na kurudisha pesa ya mwenye mali Karume jioni ya siku hiyo. Elfu mbili ama tatu anayopata inamfanya aishi yeye na mkewe na watoto wake.
Akifukuzwa barabarani na akanyang’anywa mali, anakosa kazi ya kufanya na analazimika kumtumikia bosi mwenye mali mpaka atakapofidia mali iliyopotea bila kupata cha juu. Shida na madhila anayoyapata bwana Kalumanzila zinaniumiza na kunigusa sana moyoni, hata kama yeye si mjomba wangu.
Tarehe 4, Agosti 2014, Rais Kikwete akihutubia kwenye Kituo cha kimataifa cha maendeleo (Center for Global Development) alisema: “…Nataka na natamani kuwa Rais wa mwisho wa Tanzania kuongoza nchi masikini.
Raslimali ya gesi inatoa nafasi na fursa kubwa kwa nchi yetu kuondokana na umasikini. Mimi nimeongoza nchi masikini, lakini nataka mrithi wangu kuongoza nchi yenye ustawi na utajiri…” Mimi nasema hivi: nataka na natamani kuwa Rais wa kwanza wa Tanzania kuongoza nchi Tajiri. Kama nitafanikiwa kuwa Rais, nitatumia miaka ya awali ya uongozi wangu kuikimbiza Tanzania kuelekea kwenye ndoto hii.
Mungu awabariki. Mungu ibariki Tanzania. Mungu ibariki Afrika.

Marekani kusaidia kupambana na Ebola 

Rais Barack Obama wa Marekani
Serikali ya Marekani imeahidi kusaidia mapambano dhidi ya Ebola.
Rais Barack Obama amesema nchi yake itapeleka vifaa vyake vya kijeshi ili kusaidia kupambana na ugonjwa huo uliozuka katika nchi za Afrika Magharibi.
Akizungumza katika kipindi cha televisheni ya NBC, nchini Marekani, Rais Obama amesema iwapo dunia haitachukua hatua za haraka, ugonjwa wa ebola utaweza kusambaa nje ya Afrika na kutishia usalama wa nchi yake.BBC

Ripoti yafichua udhalilishaji wanawake

 

Kikosi cha AMISOM, Somalia
Shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch limetoa ripoti kuhusu udhalilishwaji kijinsia wanaofanyiwa wanawake nchini Somalia na askari wa kulinda amani nchini humo.
Majeshi hayo yamo nchini Somalia yakiwakilisha Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kupambana na wapiganaji wa kikundi cha Kiislam cha Al Shaabab.
Shirika hilo la kutetea haki za binadamula Human Rights Watch limesema liliwahoji wanawake 21, wakiwemo wasichana waliobakwa na wanajeshi hao mwaka 2013.
Visa vingi vimeripotiwa katika kambi zinazosimamiwa na wanajeshi wa Burundi na Uganda.
Walinda amani wa Muungano wa Afrika wamedaiwa katika ripoti hiyo, kutumia chakula cha misaada kushawishi wasichana na wanawake kufanya mapenzi nao.
Wanajeshi hao wanadaiwa pia kuwabaka ama kuwadhalilisha kingono wanawake waliofika katika kambi hizo kuomba msaada wa matibabu au maji.BBC

BENKI KUU YA TANZANIA IMETOA TOLEO JIPYA LA SARAFU YA SHILINGI 500‏ 


Sarafu ya shilingi 500 itakayoanza kutumika Oktoba 2014.
BENKI Kuu ya Tanzania imetoa toleo jipya la sarafu ya shilingi 500 itakayoanza kutumika Oktoba 2014 itakayokuwa mbadala wa Noti ya shilingi 500 inayoonekana kuchakaa haraka.

Noti ya 500 inayotumika sasa.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi wa Huduma za kibenki wa benki hiyo Bw. Emmanuel Boaz wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
“Noti ya shilingi 500 hupita kwenye mikono ya watu wengi zidi na ndiyo inayotumika zaidi kwenye manunuzi ya kawaida hivyo kuchakaa haraka ndio maana tumeamua kutoa toleo la sarafu itakayoanza kutumika mapema mwezi wa 10 mwaka huu.”alisema Boaz.
Akifafanua zaidi Boaz amesema Sarafu hukaa kwenye mzunguko kwa miaka mingi zaidi kuliko noti na pia noti zimekuwa zilikaa katika mzunguko kwa muda mrefu bila kurejeshwa kwenye mabenki kwa wakati muafaka ili zibadilishwe.(P.T)
Akitaja sifa za sarafu hiyo mpya Boaz amesema kwanza umbo lake ni la duara lenye michirizi pembezoni na kipenyo cha milimita 27.5 na uzito wa gramu 9.5.
Sifa nyingineni kuwa ina rangi ya fedha na imetengenezwa kwa madini aina ya chuma na Nickel na kwa upande wa mbele ina sura ya Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Sheikh Abeid Aman Karume na kwa nyuma ina taswira ya mnyama nyati akiwa mbugani.
Pia Boaz alibainisha kuwa sarafu hiyo kwa upande wa nyuma ina kivuli kilichojificha ambacho huonesha thamani ya sarafu ya 500 au neno BOT inapogeuzwa geuzwa.
Kwa upande wa matumizi Boaz amesema sarafu hiyo itakapoanza kutumika itatumika sambamba na noti za shilingi 500 hadi zitakapokwisha kwenye mzunguko.
Benki Kuu ya Tanzania ndiyo chombo chenye jukumu la kutoa sarafu na noti halali (legal tender) zinazotumika nchini ambapo katika kutimiza jukumu hili Benki kuu hutengeneza noti na sarafu zenye uwiano mzuri wa thamani (denomination) unaozingatia uwezekano wa zile zenye thamani kubwa kuweza kugawika katika zile zenye thamani ndogo.